Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Wanasayansi Chipukizi (Young Scientists Tanzania - YST) limetangaza kuwa jumla ya miradi 45 ya kisayansi imechaguliwa kushiriki katika Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi yatakayofanyika Septemba 18, 2025 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Tunataka kuona vijana wakitumia sayansi kutatua changamoto halisi za jamii. Miradi itakayowasilishwa pia inagusa matumizi ya AI katika uchunguzi wa kitabibu, uboreshaji wa mifumo ya umeme na mifereji ya maji, sambamba na utunzaji wa mazingira,” alisema Dk. Kamugisha.
Aliongeza kuwa lengo la kufanya mashindano hayo UDSM ni kuwaunganisha wanafunzi wabunifu kutoka shule za sekondari na wanasayansi wabobezi kutoka vyuo vikuu ili kupata ushauri wa kitaalamu na kuendeleza gunduzi zao.
Kwa mujibu wa Kamugisha, mgeni rasmi katika hafla hiyo atakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Karimjee Foundation (KFI), Caren Rowland, ambao kwa kushirikiana na Toyota Tanzania wamekuwa wadhamini wakuu wa YST tangu mwaka 2012, alisema wameendelea kusaidia washindi kwa ufadhili wa elimu ya juu.
“Tangu tuanze udhamini, tumeshafadhili wanafunzi 49 na mwaka huu tunaongeza wanne zaidi kufikisha jumla ya wanafunzi 53 waliopata nafasi ya elimu ya juu kupitia mpango huu. Baadhi yao wameshahitimu, wengine wako vyuoni na wapo wanaoendelea hadi ngazi ya uzamili na uzamivu,” alisema Rowland.
Naye Ramlat Hamad, mshindi wa jumla wa mashindano hayo mwaka mmoja uliopita kutoka Shule ya Sekondari Lumumba, Zanzibar, alisema mpango huo umebadilisha maisha yake na ya wanafunzi wengi.
“YST na Karimjee Foundation wamenisaidia kutimiza ndoto ya elimu ya juu. Leo hii ninaendelea na masomo yangu nikiwa na uhakika wa kufikia malengo makubwa zaidi,” alisema Ramlat.
Mashindano ya YST mwaka huu yanatarajiwa kuvutia washiriki na wadau kutoka mikoa yote ya Tanzania, huku yakitoa fursa kwa vijana kuonesha ubunifu wao katika sayansi na teknolojia kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
No comments:
Post a Comment