Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw.Crispin Chalamila (kushoto) akiwa na Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Bw. Majaba Magana (kulia) wakionesha hati ya makubaliano ya kubadilishana taarifa (Data Sharing Agreement) mara baada ya kusaini Makubaliano hayo ,hafla iliyofanyika leo Septemba 24,2025 katika makao makuu ya TAKUKURU jijini Dodoma.
Na Alex Sonna, Dodoma.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) zimesaini hati ya makubaliano ya kubadilishana taarifa (Data Sharing Agreement), hatua inayolenga kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na uhalifu wa kifedha nchini.
Hafla ya utiaji saini imefanyika jana, Septemba 24, 2025, katika Makao Makuu ya TAKUKURU jijini Dodoma na kushuhudiwa na viongozi wakuu wa taasisi hizo — Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila na Kamishna wa FIU, Majaba Shabani Magana, pamoja na wakurugenzi na maafisa waandamizi.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Bw. Chalamila alisema makubaliano hayo mapya ni mwendelezo wa ushirikiano ulioanza tangu mwaka 2015, ambapo taasisi hizo zilisaini makubaliano ya awali ya kushirikiana katika masuala ya uchunguzi wa rushwa na uhalifu wa kifedha.
“Makubaliano haya ya kubadilishana taarifa ni utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2023, ambayo inazitaka taasisi zinazoshirikiana kuhakikisha zinasaini Data Sharing Agreement endapo zitahusiana katika kubadilishana taarifa,” alisema Bw. Chalamila.
Aliongeza kuwa lengo kuu ni kurahisisha na kuongeza ufanisi wa uchunguzi na udhibiti wa vitendo vya rushwa na utakatishaji fedha kwa kutumia taarifa sahihi na za haraka.
Kwa mujibu wa Chalamila, kati ya mwaka 2022 na 2025, TAKUKURU imepokea taarifa 47 za miamala yenye mashaka kutoka FIU, ambapo 36 zilifanyiwa uchunguzi. Aidha, kuanzia 2023 hadi 2025, taasisi hiyo iliomba taarifa 141 kutoka FIU kwa ajili ya kusaidia uchunguzi mbalimbali.
“FIU imekuwa msaada mkubwa katika kufanikisha uchunguzi wetu. Ushirikiano huu umewezesha chunguzi kufanyika kwa haraka na kutoa matokeo chanya,” alisisitiza.
Aliwataka pia wadau wengine kuendelea kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano hayo, akibainisha kuwa tatizo la rushwa haliwezi kutokomezwa bila ushiriki wa Watanzania wote.
“Tunasisitiza kila mmoja atimize wajibu wake. Kaulimbiu yetu inasema: Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu,” alisema Chalamila.
Kwa upande wake, Kamishna wa FIU, Majaba Magana, alisema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kushughulikia changamoto za ukosefu wa mfumo wa kitaifa wa kielektroniki wa kuhifadhi na kusoma takwimu za uhalifu wa kifedha.
“Hapo awali kulikuwa hakuna muunganiko wa moja kwa moja wa takwimu, jambo lililosababisha ugumu wa kupata picha kamili ya mwenendo wa uhalifu wa kifedha nchini. Hii sasa itarahisisha kazi na kuongeza ufanisi,” alisema Magana.
Makubaliano haya yanatajwa kuwa msingi wa kuimarisha zaidi jitihada za serikali na taasisi zake katika kudhibiti mianya ya rushwa na biashara haramu ya fedha, kwa kushirikiana kitaasisi na kutumia teknolojia ya kisasa.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw.Crispin Chalamila (kushoto) akiwa na Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Bw. Majaba Magana (kulia) wakisani hati ya makubaliano ya kubadilishana taarifa (Data Sharing Agreement), hafla iliyofanyika leo Septemba 24,2025 katika makao makuu ya TAKUKURU jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw.Crispin Chalamila (kushoto) akiwa na Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Bw. Majaba Magana (kulia) wakibadilishana hati ya makubaliano ya kubadilishana taarifa (Data Sharing Agreement) mara baada ya kusaini Makubaliano hayo ,hafla iliyofanyika leo Septemba 24,2025 katika makao makuu ya TAKUKURU jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw.Crispin Chalamila,akizungumza mara baada ya kusaini hati ya ya makubaliano ya kubadilishana taarifa (Data Sharing Agreement) kati ya TAKUKURU na FIU,hafla iliyofanyika leo Septemba 24,2025 katika Makao Makuu ya TAKUKURU jijini Dodoma.

Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Bw. Majaba Magana,akizungumza mara baada ya kusaini hati ya Makubaliano ya kubadilishana taarifa (Data Sharing Agreement) kati ya FIU na TAKUKURU ,hafla iliyofanyika leo Septemba 24,2025 katika Makao Makuu ya TAKUKURU jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment