HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 1, 2025

JKT Yasherehekea Miaka 61 kwa Kupanda Miti na Kuchangia Damu

 

MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele,akiwaongoza Maafisa ,Askari na Vijana kupanda miti katika maeneo yanayozunguka Makao Makuu ya JKT, pamoja na kuchangia damu katika Hospitali ya Uhuru, Chamwino jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 61 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu kuasisiwa kwake Septemba 1, 1964.

Na Alex Sonna, Chamwino.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeadhimisha miaka 61 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kupanda miti na kuchangia damu katika Hospitali ya Uhuru, Chamwino jijini Dodoma.

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, aliwaongoza maafisa, askari na vijana wa JKT kushiriki katika shughuli hizo za kijamii leo Septemba 1, 2025, akitoa wito kwa taasisi mbalimbali nchini kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wananchi wanaohitaji huduma hiyo muhimu.

Kwa maelekezo ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, vikosi vyote vya JWTZ viliadhimisha siku hiyo kwa kufanya shughuli za kijamii ikiwemo upandaji miti, usafi na uchangiaji damu.

“Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni mali ya wananchi, hivyo katika sherehe hizi lazima turudi kwa jamii. Sisi JKT tumeona tujitolee damu kwa wahitaji tukitambua uhitaji ni mkubwa,” alisema Meja Jenerali Mabele.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kambi ya Makao Makuu ya JKT, Kanali Geofrey Mvula, alisema pia elimu ilitolewa kwa maafisa na vijana kuhusu umuhimu wa kuchangia damu, jambo lililohamasisha wengi kushiriki.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Uhuru, Devotha Rweyemamu, aliushukuru uongozi wa JKT kwa msaada huo akibainisha kuwa hospitali hiyo inapokea wagonjwa wengi wa ajali na wenye uhitaji wa damu, hivyo msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha.
            

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad