HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 17, 2025

Ilani ya Uchaguzi CCM inagusamaisha ya watu, wataichagua


NA MWANDISHI WETU, MBEYA

MAKAMU MMwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema Watanzania wataichagua CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuwa Ilani yake ya Uchaguzi inagusa maisha na maendeleo yao.

Amesema hakuna chama chochote cha siasa miongoni mwa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo ambacho kimejipanga kufanya mambo mazuri kama ilivyo CCM, hivyo wananchi hawataona sababu ya kuvichagua.

Wasira alieleza hayo jana mjini Mbeya alipozungumza na viongozi wa Chama kutoka majimbo ya Mbeya mjini na Uyole, alipokuwa akimwombea kura Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan na kuweka mikakati ya ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu

"Yako mambo mengi tumedhamiria kuyafanya kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2030 kwa manufaa ya wananchi.

"Elimu tumekubaliana tubadili mfumo wa elimu ili kijana akienda sekondari 'school' (shule ya sekondari) akitoka anajua ujuzi wa kazi. Tumeeneza umeme, tunapeleka maji, ukiwa na maji ya bomba endapo bomba likiharibika unafanyaje, lazima uwe na watu hapo mtaani kwako ambao wanaweza kurekebisha bomba na ndio kazi yao watakuwa wamesoma," alisema.

Alisema kutokana na kazi kubwa inayofanyika kutanua fursa mbalimbali ikiwemo ya kusambaza umeme, ni muhimu kuwa na mafundi wenye uwezo wa taaluma za umeme hadi vijijini na hiyo ni moja ya sababu za kubadili mfumo wa elimu uendane na mahitaji ya wakati.

"Tumesema katika Ilani hii vijana wasome, waanzishe kampuni zao zinazoendana na ujuzi wao na sisi tuwape mitaji waweze kufanya kazi ya kujiajiri na kuajiri wenzao na hii wamefanya Korea Kusini na wameweza, kwa nini sisi hatuwezi," alieleza.

Kwa mujibu wa Wasira, CCM inakusudia kuimarisha zaidi huduma za afya, kuwapa bima Watanzania wote wenye uwezo na wasiokuwa nao na kwamba sasa Bunge linatafuta vyanzo vya mapato kuona namna ya kugharimia bima kwa wasio lna uwezo.

Aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanafikisha kwa wananchi elimu kuhusu ahadi za maendeleo zilizomo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

"Sasa tukiyajua hayo tunaenda kwa wananchi maana mimi nawatuma nyie mwende kwa wananchi na elimu ninayowapa muipeleke kwa wananchi waelewe kumbe ndiyo mambo ya CCM haya, kumbe kuna bima, kumbe kuna elimu yenye ujuzi, kumbe maji yataongezeka," alisisitiza.


MBEYA MJINI KUNG'ARISHWA

Akizungumzia ahadi za Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa jiji la Mbeya, alisema kuhusu elimu ya msingi na sekondari inakusudia kujenga madarasa 1,600 kwa kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa inaendelea kuongezeka.

Kwenye Afya alisema zahanati 10 na vituo vya afya vitano vipya vitajengwa pamoja na kuboresha huduma.

Ili kuzidi kuling'arisha jiji hilo alisema zitawekwa taa za barabarani, "taa zile kubwa takribani 100 kwa ajili ya kuleta mwanga na tutasimamia ujenzi wa barabara za mjini kwa ajili ya kuwa na mitaa inayovutia na kama nilivyosema tutaongeza huduma ya maji pamoja na yale ambayo niliyasema kuhusu uchumi.


HAKUNA WA KUSHINDANA NA CCM

Alisema kwa sasa hakuna chama cha siasa miongoni mwa vinavyowania nafasi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambacho kina sera na ilani bora kama ya CCM.

"Sasa chama chenye sera na ilani ya kutushinda kiko wapi, maana tulipotoa hii ilani kiongozi mmoja wa chama cha siasa alitupigia simu akasema sasa CCM mmeandika mambo yote sisi tutaandika nini, nikasema hayo yetu muwe mnasoma halafu mnanukuu mnasema kama CCM ilivyosema.

Aliwahimiza wana CCM kuwauelimisha wananchi waielewe Ilani hiyo, pia kuweka mkakati wa kuhakikisha wananchi hususa wana CCM wanapiga kura.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira akimkabidhi Ilani ya Uchaguzi ya CCM Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge katika mkutano wa viongozi wa CCM kutoka Jimbo la Uyole na Mbeya Mjini, mjini Mbeya. (Pich na CCM).








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad