Na. Peter Haule na Joseph Mahumi, WF, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amelishukuru Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuimarisha uchumi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii (Extended Credit Facility – ECF) na programu ya kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (Resilient and Sustainability Facility - RSF).
Dkt. Mwamba ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa Mkutano na Ujumbe wa IMF ukiongozwa na Bw. Melesse Tashu uliofika nchini kwa ajili ya zoezi la kukagua mwenendo wa utekelezaji wa programu ya ECF na RSF.
Dkt. Mwamba alisema kuwa utekelezaji wa programu ya ECF ni wa kuridhisha, ambapo vigezo vya utendaji (Quantitative Performance Criteria) na vigezo vya kimuundo (Structural Benchmarks) vilivyolengwa kufikiwa mwezi Juni, 2025 vimetimizwa kama ilivyopangwa.
“Kufikiwa kwa vigezo vya utendaji na kimuundo, kumewezesha IMF kuidhinisha jumla ya dola za Marekani milioni 907.9 ambazo ni takribani asilimia 87 ya fedha za programu ya ECF zilizotolewa tangu kuanza kwake mwaka 2022”, alieleza Dkt. Mwamba.
Kuhusu programu ya RSF, Dkt. Mwamba alisema kuwa IMF ilitoa kiasi cha dola za Marekani milioni 345.4 katika kutekeleza programu hiyo na tayari Taifa limeanza kunufaika na utekelezaji wake.
Dkt. Mwamba alisema kuwa manufaa hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa ndoto za Tanzania kufikia malengo ya kitaifa na malengo ya kimataifa ya Mkataba wa Paris wa mwaka 2015 katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema kuwa timu hiyo ya Wataalamu kutoka IMF itakutana na Idara mbalimbali za Serikali ili kujadili maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa programu hizo.
Aidha, Dkt. Mwamba aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya programu hizo zinasimamiwa ipasavyo na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya Wataalamu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Melesse Tashu, aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa mdau mzuri wa Shirika hilo na mtekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo.
Alisema kuwa Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika utekelezaji wa Programu za ECF na RSF jambo ambalo linatoa hamasa kwa mashirika ya kimataifa kuendelea kufanya kazi na Serikali.
Bw. Tashu alisema kuwa Shirika la Fedha la Kimataifa litaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Tanzania ili kuiwezesha kufanikisha miradi muhimu yenye tija kwa wananchi wote na kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi.
Timu hiyo ya IMF iliambatana pia na Mwakilishi Mkazi wa IMF, Bw. Sebastian Acevedo, katika zoezi hilo litakalofanyika hadi Septemba 24, 2025.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akizungumza wakati akifungua Kikao kazi cha Wataalamu wa Serikali ya Tanzania na Ujumbe kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine aliishurukuru IMF kwa mchango na mwongozo endelevu katika utekelezaji wa programu ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii pamoja na programu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF).
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Sebastian Acevedo, akizungumza jambo wakati wa Kikao kazi cha Wataalamu wa Serikali ya Tanzania na Ujumbe kutoka Shirika hilo, kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.
Kiongozi wa Timu ya Wataalamu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Melesse Tashu, akizungumza jambo wakati wa Kikao kazi cha Wataalamu wa Serikali ya Tanzania na Ujumbe kutoka Shirika hilo, kilichofanyika ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma, ambapo aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwa mdau mzuri wa Shirika hilo na mtekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo.
Ujumbe wa Timu ya Wataalamu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (hayupo pichani), wakati akifungua Kikao kazi cha Wataalamu wa Serikali ya Tanzania na Ujumbe huo, kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)
Baadhi ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, wakifuatilia maelezo ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (hayupo pichani), wakati akifungua Kikao kazi cha Wataalamu wa Serikali ya Tanzania na Ujumbe kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment