MGOMBEA wa kiti cha Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani akisema ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote.
Dkt. Mwinyi aliyasema hayo leo katika mkutano mkubwa wa kampeni wa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika Uwanja wa Michezo Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja tarehe 18 Septemba 2025.
Amefafanua kuwa wananchi wana kila sababu ya kuiamini CCM kutokana na utekelezaji wa kina wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020–2025, ambayo imeleta mageuzi katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Aidha, Dkt. Mwinyi aliwahimiza wana-CCM na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi ifikapo tarehe 29 Oktoba 2025 kushiriki uchaguzi na kuipigia kura CCM ili ibaki madarakani na kuendeleza maendeleo zaidi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Taifa na Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akimnadi Dkt. Mwinyi, alimuelezea kama kiongozi sahihi, mchapakazi, msikivu na hodari, anayestahili kupewa kipindi cha pili cha kuiongoza Zanzibar ili kuimarisha zaidi kasi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment