NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetunukiwa Tuzo Kuu ya Ubunifu katika Huduma Jumuishi za Fedha (Nestor Espenilla Jr. Financial Inclusion Innovation Award) inayotolewa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI), yenye wanachama 84 duniani.
Tuzo hiyo ilipokelewa na Naibu Gavana wa BoT anayeshughulikia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, kwa niaba ya Gavana Bw. Emmanuel Tutuba, katika Mkutano Mkuu wa AFI uliofanyika hivi karibuni mjini Swakopmund, Namibia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Septemba 15, 2025 wakati akitangaza tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Lucy Shaidi, amesema ushindi huo umetokana na ubunifu wa mifumo ya malipo ikiwemo TIPS (Tanzania Instant Payment System) na TANQR (QR Code ya kitaifa ya malipo).
“Mfumo wa TIPS umesaidia kupunguza gharama za miamala kwa wananchi, huku TANQR ukiwarahisishia wafanyabiashara kupokea malipo kupitia benki na kampuni za simu. Ubunifu huu umevutia hata mataifa jirani,” amesema Lucy.
Benki Kuu tayari imeshatoa ujuzi huo kwa nchi za Kenya, Lesotho, Rwanda na Uganda, huku Burundi ikitarajiwa kufuata kwa mafunzo hivi karibuni.
Kwa mujibu wa takwimu, mfumo wa TIPS umewezesha ongezeko la miamala kufikia milioni 560 yenye thamani ya shilingi trilioni 41 katika mwaka wa fedha 2024/25.
Aidha, BoT imeanzisha mazingira ya majaribio ya ubunifu (Fintech Regulatory Sandbox Regulations, 2024) yanayowezesha wabunifu wa teknolojia kujaribu bunifu zao kabla ya kuzifikisha sokoni. Pia imezindua mfumo wa SEMA na BoT kwa ajili ya kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za kifedha.
Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Taifa, Mutashobya Mushumbusi, alisema asilimia 76 ya Watanzania kwa sasa wanapata huduma jumuishi za kifedha, huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2028.
“Tuzo hii ni heshima kubwa kwa Tanzania na inatupa motisha ya kuendelea kutumia ubunifu na teknolojia kufanikisha uchumi wa kidijitali,” amesema Mushumbusi.
Tuesday, September 16, 2025

Home
Unlabelled
BoT Yashinda Tuzo ya Kimataifa ya Ubunifu wa Huduma za Fedha
BoT Yashinda Tuzo ya Kimataifa ya Ubunifu wa Huduma za Fedha
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment