Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, amekabidhi kompyuta mpakato (laptop) 30 kwa Wakili Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Ally Possi, katika hafla fupi iliyofanyika leo, Agosti 27, 2025, katika ukumbi wa Wizara hiyo uliopo Mji wa Serikali, Mtumba – Dodoma.
Akizungumza kabla ya makabidhiano hayo, Katibu Mkuu Abdulla alisema wizara kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali imekabidhi vifaa hivyo vya TEHAMA ili kusaidia na kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake, Dkt. Possi aliishukuru Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa msaada huo, akibainisha kuwa vifaa hivyo vinakwenda kurahisisha utarahisisha utekelezaji wa majukumu ofisi hiyo kwa kiwango kikubwa hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa lipo katika mageuzi makubwa kwenye uchumi wa Kidijitali.
“Sisi mawakili wa Serikali, shughuli zetu nyingi kwa takribani asilimia 90 zinafanyika mahakamani na zinategemea matumizi ya kompyuta. Hivyo, hatua hii ya kutukabidhi vifaa hivi ni ya wakati muafaka na inaendana moja kwa moja na shughuli zetu za kila siku,” alisema Dkt. Possi.
Vilevile, Dkt. Possi aliipongeza Wizara kwa kuendelea kuwezesha mageuzi ya kidijitali nchini, ikiwemo kuhakikisha kunakuwa na gharama nafuu za huduma za intaneti kwa wananchi na taasisi.
Naye, Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo na Huduma za TEHAMA wa Wizara hiyo, Mohammed Mashaka alisema kuwa kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Serikali inaendelea kugawa vifaa vya TEHAMA kwa taasisi mbalimbali ili kurahisisha huduma, kuziunganisha taasisi hizo ili kuhakikisha huduma na rasilimali muhimu za kidijitali zinapatikana.





No comments:
Post a Comment