HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 5, 2025

WAKULIMA WILAYANI MKINGA WAHIMIZWA KUONGEZA MNYORORO WA THAMANI YA ZAO LA MWANI

Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Brigedia Jenerali Hosea Ndagala amevitaka vikundi vya Wanawake na Vijana vya wakulima wa zao la Mwani Wilayani Mkinga kuongeza mnyororo wa thamani wa zao la mwani kupitia mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo watakayoyapata.

Ametoa rai hiyo Jumatatu Agosti 04, 2025 Wilayani Mkinga katika hafla ya kufungua mafunzo ya kuvijengea uwezo wa kilimo bora, usimamizi wa vikundi, usimamizi wa fedha,utunzaji kumbukumbu, kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao pamoja na masoko ya zao la mwani yanayo ratibiwa na Chuo cha Mipango kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa ufadhili wa Serikali ya Japan pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

“Ndugu washiriki, Wilaya ya Mkinga ni miongoni mwa Wilaya zenye fursa kubwa katika sekta ya kilimo cha mazao ya bahari hususani uzalishaji wa zao la mwani, hivyo nitumie fursa hii kuwahimiza washiriki wa mafunzo haya ambayo nimeambiwa yatafanyika kwa takribani siku kumi na tano kwa nadharia na vitendo. Ninaomba myazingatie maarifa haya yakawe chachu ya ongezeko la mnyororo wa thamani wa zao letu la mwani ili likidhi ubora wa soko la kimataifa.” Alisema Brigedia Jenerali Ndagala.

Aidha, Brigedia Jenerali Ndagala ameishukuru Serikali ya Japani na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha ulinzi na usalama katika ukanda wa Bahari ya Tanzania pamoja na eneo la maziwa makuu.

Nae, Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Veronica Sigara amesema Shirika limedhamilia kuhakikisha linashirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia uchumi wa bluu kwa kuwalenga makundi ya wanawake na vijana katika ukanda wa pwani ya Tanzania.

Kwa upande wake Katibu Tarafa wa Mkinga Bw. Valentino Mkinga akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mkinga ameahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa vikundi na wawezeshaji wa mafunzo haya ambayo yatatatua changamoto zinazovikabili vikundi vya wakulima wa zao la mwani wa Wilaya ya Mkinga.

Kwamujibu wa Mratibu wa Mafunzo haya ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Mipango Dkt. Bonamax Mbasa amesema kuwa mafunzo haya kwa vikundi hivi ni sehemu ya utekelezaji wa mwongozo wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika bahari na maziwa makuu kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo hayo uliozinduliwa Februari 2023 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) ambapo sehemu ya kwanza ulitekelezwa katika Wilaya tatu ikiwa ni pamoja na Mafia, Pangani na Bagamoyo ambazo shughuli zake kuu za kiuchumi zinategemea mazao ya bahari.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad