Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima akizungumza katika Mkutano wa Tume, Wahariri na Waandishi wa Habari, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Agosti 4, 2025 ambapo amewakikishia washiriki hao kuwa, ofisi yake itafanya kazi kwa karibu katika kipindi cha uchaguzi mkuu kwa njia mbalimbali ikiwemo kushiriki katika vipindi vya redio na runinga na kutoa taarifa kwa wakati.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima akizungumza katika Mkutano wa Tume, Wahariri na Waandishi wa Habari, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Agosti 4, 2025 ambapo amewahakikishia washiriki hao kuwa, ofisi yake itafanya kazi nao kwa karibu katika kipindi cha uchaguzi mkuu kwa njia mbalimbali ikiwemo kushiriki katika vipindi vya redio na runinga na kutoa taarifa kwa wakati.
Na Avila Kakingo
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imevitambua vyombo vya habari kuwa ni wadau muhimu katika kuhakikisha mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unafanyika kwa uwazi, amani na ufanisi, huku ikisisitiza wajibu wao katika kuelimisha, kushirikisha na kutuliza jamii.
Akizungumza leo Agosti 3, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, amesema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kujenga uelewa wa umma kuhusu hatua mbalimbali za uchaguzi.
"Tunategemea vyombo vya habari kama daraja kati ya Tume na wananchi. Habari zenu ni dira kwa wapiga kura. Zitolewe kwa usahihi, kwa wakati na kwa uwajibikaji mkubwa," amesema Kailima katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa Mlimani City.
Ameongeza kuwa vyombo hivyo vimekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya mpiga kura na kueleza hatua muhimu za mchakato wa uchaguzi, hivyo Tume itaendelea kushirikiana navyo kwa karibu kupitia vipindi vya redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii.
Kailima amewataka waandishi kuzingatia maadili ya taaluma, uwiano wa taarifa, na kujiepusha na kuripoti habari zenye misingi ya upotoshaji, upendeleo au uchochezi wa hofu kwa wananchi.
“Mnapaswa kuwa sauti ya kutuliza, si kuchochea. Taarifa zenu zitoe mwelekeo sahihi kwa jamii. Hii ni nafasi ya kuonyesha ubobezi wa taaluma yenu kwa maslahi ya taifa,” alisisitiza.
Akiwasilisha ratiba ya uchaguzi, Kailima amesema utoaji wa fomu kwa wagombea wa Urais na Makamu wa Rais utaanza Agosti 9 hadi 27, huku Uchaguzi Mkuu ukitarajiwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Katika kuhakikisha mazingira rafiki ya kazi kwa wanahabari, Tume imetangaza kuwa kuanzia Septemba 1 hadi 30, itafanya usajili rasmi wa waandishi wa habari na vyombo vyao, hatua itakayowezesha utoaji wa vitambulisho maalum kwa kurahisisha kazi siku ya uchaguzi.
Aidha, washiriki wa mafunzo hayo watapatiwa nakala za sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya uchaguzi ili kuhakikisha wanazingatia viwango vya kitaaluma na kisheria katika uandishi wao.
Kailima alihitimisha kwa kuwataka waandishi kutumia vyema mafunzo hayo kwa kuuliza maswali, kushirikiana na kujifunza kwa kina ili wawe mabalozi wa amani, ukweli na mshikamano kuelekea uchaguzi huo.
Kaulimbiu ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni: “KURA YAKO, HAKI YAKO – JITOKEZE KUPIGA KURA.”
No comments:
Post a Comment