HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, August 9, 2025

TVLA YANG’ARA NANENANE 2025, YANYAKUA TUZO YA 5 KITAIFA NA KANDA

Na Daudi Nyingo - Dodoma

Agosti 8, 2025 Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imepata heshima kubwa kitaifa baada ya kutunukiwa Tuzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, baaada ya kuibuka Mshindi wa Kwanza kwa Wakala wa Serikali wanaotoa huduma za uzalishaji bora na zenye tija kwa sekta ya mifugo nchini kwenye maonesho ya nanenane kitaifa yaliyofanyika katika uwanja wa Nzuguni Mkoani Dodoma kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 8 Agosti, 2025.

Mbali na ushindi huo wa kitaifa, TVLA pia iliibuka kidedea katika ngazi za kanda kwa kwa kupata nafasi za juu katika maonesho mbalimbali ya Nanenane yaliyofanyika nchini. Katika Kanda ya Ziwa Magharibi, maonesho yaliyofanyika Uwanja wa Nyamhongolo mkoani Mwanza, TVLA iliibuka Mshindi wa Kwanza kwa kipengele cha Taasisi za Uchunguzi Maabara, tuzo ambayo ilikabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda. Vilevile, katika Kanda ya Kusini, kwenye maonesho yaliyofanyika Uwanja wa Ngongo mkoani Lindi, TVLA ilipata Nafasi ya Tatu kwa kipengele cha Taasisi za Huduma za Utafiti, tuzo iliyotolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo.

Ufanisi huo uliendelea katika Kanda ya Ziwa Mashariki, ambapo TVLA ilipata Nafasi ya Pili kwa kipengele cha Kundi la Taasisi za Umma kwenye maonesho yaliyofanyika Uwanja wa Nyakabindi mkoani Simiyu, tuzo ikikabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi. Kadhalika, katika Kanda ya Magharibi, kwenye maonesho yaliyofanyika Uwanja wa Fatma Mwasa mkoani Tabora, TVLA ilishinda Nafasi ya Pili kwa kipengele cha Taasisi za Serikali zinazotoa huduma za uzalishaji, tuzo hiyo ikitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP (Mst.) Balozi Simon Sirro.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dkt. Stella Bitanyi, alisema kuwa;

“Kupata tuzo tano katika ngazi ya kitaifa na kanda ni jambo la heshima na fahari kwa TVLA. Ushindi huu ni matokeo ya kazi kwa bidii ya watumishi wetu wote, uwekezaji wa serikali na uongozi makini wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya mifugo. Tuzo hizi zinatupa hamasa ya kuendelea kuboresha huduma zetu za kitaalamu, ubunifu katika tafiti na uchunguzi wa magonjwa, pamoja na kusaidia wafugaji kuongeza tija na kipato chao.”

“Tumethibitisha kuwa TVLA ni nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta ya mifugo nchini, tutauhakikisha wafugaji wanapata huduma bora zaidi.” Alisema Dkt. Bitanyi.

Dkt. Bitanyi alisisitiza kuwa TVLA itaendeleza mikakati ya kitaalamu na teknolojia za kisasa ili kuhakikisha huduma zake zinaendelea kuisaidia Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye mifumo bora ya afya ya wanyama barani Afrika.








Mshindi wa Pili (Taasisi za Umma) – Maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Mashariki, Uwanja wa Nyakabindi mkoani Simiyu. Tuzo ilikabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, Agosti 8, 2025.


Mshindi wa Tatu (Taasisi za Huduma za Utafiti) – Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, Uwanja wa Ngongo mkoani Lindi. Tuzo ilikabidhiwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo, Agosti 8, 2025.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad