HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, August 9, 2025

TBL Plc YAAHIDI KUENDELEZA SEKTA YA KILIMO, YAWEZESHA WALIMA KUPITIA MAFUNZO,UBIA WA KIMKAKATI NA MASOKO


 TANZANIA Breweries Plc (TBL Plc), mwanachama wa familia ya AB InBev, imedhihirisha upya dhamira yake ya muda mrefu ya kuendeleza sekta ya kilimo nchini Tanzania, kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane 2025 yaliyofanyika kitaifa mkoani Dodoma. 

Kupitia kaulimbiu ya “Shangwe kwa wakulima ”TBL Plc inadhirisha kuwa si kinara wa utengenezaji wa vinywaji pekee bali pia ni mshirika wa kuaminika wa wakulima zaidi ya 2,500 nchini.

Kwa kuzingatia mkakati wake wa uendelevu na dira ya kujenga mustakabali wenye mafanikio kwa wote, TBL Plc. imeimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo kupitia ushirikiano wa moja kwa moja na wakulima wanaosambaza malighafi muhimu kama mtama, shayiri na mahindi, na mazao muhimu katika utengenezaji wa vinywaji vyake. 

Kupitia mpango wake wa Local Content Sourcing, kampuni imehakikisha ununuzi wa malighafi unafanyika ndani ya nchi, hatua inayochangia kuinua uchumi wa vijijini, kuongeza ajira na kupunguza utegemezi wa uagizaji malighafi kutoka nje. 

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL Plc. Michelle Kilpin, alisema:“ Wakulima kwetu si wasambazaji wa malighafi pekee bali ni wadau wetu wa maendeleo. Tunajivunia kushirikiana na maelfu ya wakulima nchini, tukiwapatia masoko, vifaa, mafunzo na msaada wanaohitaji ili kufanya kilimo kwa njia endelevu.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano ya Kampuni wa TBL Plc, Neema Temba, aliongeza: “Tunaamini mkulima anapofanikiwa, sote tunafanikiwa. Ndiyo maana tunawekeza katika kuimarisha mfumo wa kilimo nchini. Kupitia ushirikiano huu wa kimkakati; tunahakikisha zaidi ya wakulima 4,500, wanapata mafunzo, ushauri wa kitaalamu na masoko ya uhakaika kuongeza uzalishaji na endelevu.”

Kama sehemu ya dhamira hiyo, hivi karibuni TBL Plc. iliandaa “Siku ya Wakulima wa Mtama”, tukio la kwanza la aina yake lililokutanisha mamia ya wakulima, wataalamu wa kilimo na wadau wakuu mbalimbali kujadili mchango wa zao la mtama katika kukuza kilimo endelevu na usalama wa chakula. 

Tukio hilo lilihusisha kutambua mchango wa wakulima, kubadilishana maarifa, kukabidhi vifaa vya kilimo, na kuonyesha namna TBL inavyohakikisha soko la mazao yanayozalishwa na wakulima hao. 

Mpango wa TBL Plc wa Kusaidia Wakulima Unajumuisha Mafunzo juu ya mbinu bora za kilimo, afya ya udongo na mbinu za kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi, Upatikanaji wa vifaa vya kilimo kupitia ubia wa kimkakati na wasambazaji pamoja na taasisi za kifedha na  Soko la uhakika na malipo ya wakati kwa mazao yanayotumika kwenye utengenezaji wa vinywaji.

Wakulima wengi wanaonufaika na mpango huo  wanatoka katika maeneo yaliyo hatarini kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo Dodoma, Arusha, Kilimanjaro Magharibi na Manyara. Kwa kuunganisha ubunifu na uendelevu katika mfumo wake wa kilimo, TBL Plc inawawezesha wakulima wadogo kuongeza ustahimilivu, kutumia teknolojia bora na kuinua kipato chao.

Mikakati ya TBL Plc inalingana na ajenda ya Serikali ya Tanzania ya kukuza kilimo na viwanda. Kampuni inaendelea kushirikiana na serikali za mitaa, vyama vya wakulima na washirika wa maendeleo kuhakikisha manufaa ya muda mrefu.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad