Timu ya Nyasubi FC kutoka Kahama imetwaa ubingwa wa mashindano ya Mapung’o Cup 2025 baada ya kuichapa Nyakagwe FC ya Geita kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliopigwa leo, Agosti 22, 2025, kwenye uwanja wa Soko la Jumatano, Nyakagwe.
Kwa kutwaa ubingwa huo, Nyasubi FC imejinyakulia zawadi ya shilingi milioni 5 na kuandika historia mpya kwenye mashindano hayo yaliyoshirikisha jumla ya timu 12 kutoka mikoa ya Mwanza, Geita na Shinyanga.
Mashindano hayo yalidhaminiwa na mdau wa michezo Pascal Mapung’o maarufu kama King Mapung’o, ambaye pia ndiye mratibu mkuu wa Mapung’o Cup.
Akizungumza baada ya ushindi huo, kocha wa Nyasubi FC alisema kuwa wachezaji wake wametekeleza maagizo ipasavyo na kuahidi kuendelea kuibeba timu hiyo kwenye mashindano mengine makubwa.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Geita, Elisha Simba, alimpongeza mratibu na waandaaji wa mashindano hayo akisema yamekuwa chachu kubwa ya kuinua na kuibua vipaji vya vijana katika mchezo wa soka.
No comments:
Post a Comment