Mkutano huo ulifungwa rasmi na Waziri Mkuu wa Japan Mheshimiwa Shigeru Ishiba na Rais wa Angola na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Mheshimiwa João Lourenço.
Mkutano huo umepitisha Azimio la Yokohama lililobeba maeneo mahsusi kwa nchi wanachama wa AU na Japan kuimarisha ushirikiano kwa kipindi cha Agosti 2025 hadi Agosti 2028 katika maeneo makuu matatu ya Uchumi, Jamii na Amani na Usalama.
Katika sekta ya uchumi, Japan imeahidi uwekezaji wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 7, ikiwemo mpango wa EPSA wa kukuza sekta binafsi barani Afrika, uwekezaji kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) na kuimarisha biashara kupitia Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).
Katika sekta ya jamii, Japan imetangaza kuwekeza kwenye afya, elimu, na mafunzo kwa zaidi ya vijana 300,000 wa Afrika, sambamba na ufadhili wa Dola milioni 550 kwa usambazaji wa chanjo kupitia GAVI na kusaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Katika eneo la amani na usalama, Japan itaendeleza ushirikiano na AU katika kuimarisha taasisi za sheria, kutoa mafunzo ya utatuzi wa migogoro na kuhamasisha ushiriki wa vijana na wanawake katika ajenda za amani.
Tanzania itaendelea kutumia fursa hiyo na kuimarisha ushirikiano wake wa kidiplomasia na wa kihistoria na Japan katika maeneo makuu matatu ya TICAD kwa ajili ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kwa manufaa mapana ya Tanzania.















No comments:
Post a Comment