HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 4, 2025

Mahakama Yabariki Mashahidi wa Kesi ya Uhaini Dhidi ya Lissu Kulindwa

 

MAHAKAMA Kuu ya Masijala ya Dar es Salaam imekubali ombi la upande wa Jamhuri la kuficha majina na taarifa nyingine za mashahidi raia wa upande wa Mashitaka katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.

Akisoma uamuzi huo leo, Agosti 4, 2025, Jaji Hussein Mtembwa amesema kutokana na uzito wa kosa la uhaini na hofu ya mashahidi kutishiwa, ni haki kwa mashahidi raia kulindwa kwa kutotajwa majina yao, anuani wala mahali walipo katika hatua ya committal, Preliminary Inquiry (PI) na hata wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Jaji Mtembwa amesema kwa mujibu wa kiambatanisho kilichowasilishwa na upande wa mashtaka, kesi inayomkabili mshtakiwa katika Mahakama ya Kisutu inahusu uhaini. Akifafanua zaidi, amesema kwa kuwa mshtakiwa ana wafuasi wengi ndani na nje ya nchi, na kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa na ACP Amini Mahamba kuwa mashahidi hao wanatishiwa na watu wa karibu na mshtakiwa ili wasitoe ushahidi mahakamani, usalama wao unaweza kuwa hatarini.

"Nilichokiona ni kwamba kosa la mshtakiwa ni kati ya makosa makubwa, na pili, mashahidi hawa wanaotarajiwa kwa kiapo cha ACP Mahamba ni kwamba wanatishiwa... Sisi kama Mahakama tukifikia hapo, tutaangalia Sheria inasemaje," amesema Jaji.

Ameongeza kuwa Sheria inaruhusu kuwalinda mashahidi na watoa taarifa, hasa pale ambapo wao au familia zao wako katika hatari ya kudhuriwa, ingawa pia inapaswa kuzingatiwa kuwa mshtakiwa ana haki ya kumuona na kumhoji shahidi.

"Mahakama ina wajibu wa kulinganisha haki zote mbili kwa uwiano kwa lengo la kutenda haki. Nimeamua kukubali maombi ya kuficha mashahidi ambao ni raia tu," amesema.

Hata hivyo, Mahakama imekataa ombi la Jamhuri la kuficha taarifa za mashahidi wote bila kujali uraia, na kueleza kuwa mashahidi ambao si raia wataendelea kutoa ushahidi kwa kawaida na kwa majina yao halisi.

"Kama shahidi si raia, atatoa ushahidi katika hali ya kawaida kwa kuonekana na bila kufichwa jina au taarifa nyingine zinazomhusu," amesema.

Aidha, Mahakama imeiagiza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuandaa utaratibu wa kuchuja (screen) taarifa zote zitakazowasilishwa mahakamani ili kuondoa zile zinazoweza kufichua utambulisho wa mashahidi raia.

Pia, Mahakama imesema vyombo vya habari havitaruhusiwa kuchapisha au kutangaza taarifa yoyote inayoweza kufichua utambulisho wa mashahidi hao bila kibali cha Mahakama.

"Wakati wa committal, PI na hata wakati wa usikilizwaji, suala la kuchapisha au kusambaza taarifa zenye majina ya mashahidi wa upande wa mashtaka limepigwa marufuku. Haina maana unaficha mahakamani halafu chombo cha habari kinamtaja shahidi. Vyombo vya habari vitaruhusiwa kufanya hivyo tu kwa kupata kibali cha Mahakama," amesema.

Mahakama imekazia kuwa hairuhusiwi kusambaza au kuchapisha taarifa yoyote inayoweza kufichua jina, makazi, ndugu, marafiki au watu wa karibu wa mashahidi hao isipokuwa kwa ruhusa maalum kutoka kwa Mahakama.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad