
Na Mwandishi Wetu, Bukoba
Shule ya Sekondari ya Wasichana Josiah imeadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwake kwa Ibada Kuu ya Shukrani iliyoongozwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Malasusa.
Katika mahubiri yake, Askofu Malasusa alisema mafanikio ya shule hiyo yametokana na msingi wa maadili mema na imani kwa Mungu. “Mungu hayuko mbali na shule hii na atawasimamia na kuhakikisha wanashinda kwa kuwa Yeye amejaa neema. Hata sasa Bwana amesaidia,” alisema.
Alisisitiza kuwa shule za Tanzania zinapaswa kuzingatia malezi ya kimaadili sambamba na elimu ya darasani, ili kujenga kizazi bora chenye uzalendo na uadilifu.

Shule ya Josiah, iliyoanzishwa mwaka 2010 katika Kata ya Ijuganyundo, Manispaa ya Bukoba, imekuwa kimbilio kwa wazazi na walezi kutokana na elimu bora na malezi yenye maadili. Mjumbe wa Bodi ya Shule na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dkt. Abednego Keshomshahara, alisema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa na kuwa mfano wa kuigwa kwa shule binafsi nchini.
Kwa upande wake, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, alipongeza uongozi wa shule kwa kujitolea bila kuchoka na kuendeleza malezi yenye misingi ya maadili. “Nafurahi kuona shule hii imesimama kwa imani na uadilifu, imekuwa chombo cha kujenga jamii yenye maadili mema na kuandaa viongozi wa kesho,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima, aliahidi ushirikiano wa karibu kati ya serikali na taasisi binafsi za elimu ili kuboresha miundombinu na kuongeza ubora wa elimu. “Serikali iko tayari kushirikiana na wadau wa elimu kama Josiah Girls’ Secondary School katika kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu bora na mazingira salama ya kusomea,” alisema.
Mbali na ibada na hotuba za viongozi, maadhimisho hayo yalihusisha utoaji wa tuzo kwa wadau waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya shule, pamoja na shuhuda kutoka kwa wanafunzi na wahitimu waliothibitisha ubora wa malezi na elimu waliyoipata.
Kwa jumuiya ya Josiah Girls’ Secondary School, miaka 15 ni ishara ya baraka, mshikamano na matumaini ya mafanikio makubwa zaidi katika siku zijazo, ikiwa na dira ya “Ndoto Yangu, Upeo Wangu” inayoendelea kuongoza kila hatua ya safari yake ya kielimu.
Wageni waalikwa wakifuatilia.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Josiah Girls wakitoa burudani kwa wageni waalikwa.
Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini (katikati) akifuatilia utoaji wa zawadi kwa wafanyakazi.



Zawadi za vyeti zikitolewa kwa wafanyakazi na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Malasusa (kulia).

Picha ya pamoja ya viongozi wa dini na serikali.
No comments:
Post a Comment