Na Mwandishi Wetu, Morogoro
BAADHI ya wakazi wa Kata ya Tungi katika Manispaa ya Morogoro wameeleza namna kisima cha maji kilichojengwa kwa ufadhili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Abdulaziz Abood, kilivyokuwa mkombozi wa huduma ya maji katika eneo hilo.
Wameyasema hayo leo Julai 5, 2025 kwa nyakati tofauti kufuatia taarifa zilizoibuka mitandaoni hivi karibuni zikidai kuwa kisima hicho hakijawahi kutoa maji tangu kuzinduliwa, madai ambayo wakazi hao wameyataja kuwa ni ya kupotosha na yasiyo na ukweli wowote.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari, wananchi hao ikiwemo Hamida Hussein na Tuhuma Ramadhani Yusuphy wamesema kisima hicho kimekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza adha ya upatikanaji wa maji safi na salama, si tu kwa wakazi wa maeneo ya jirani, bali pia kwa wagonjwa na wahudumu katika Kituo cha Afya Tungi.
"Kabla ya kisima hiki tulikuwa tunahangaika sana kutafuta maji, lakini sasa huduma imeimarika. Tunaomba watu wasitumie mitandao ya kijamii kupotosha ukweli," alisema Hamida Hussein
Katika hatua nyingine, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Tungi, Dkt. Maziku Samson Kapambala amethibitisha kuwa kisima hicho kimeboresha kwa kiasi kikubwa huduma za afya kituoni hapo.
"Kisima hiki kimesaidia sana katika shughuli zetu za kila siku, hasa katika kuhakikisha usafi wa mazingira, huduma kwa wagonjwa, na matumizi mengine ya kitabibu. Kulikuwa na hitilafu ya muda mfupi ya umeme, lakini huduma ya maji imeendelea vizuri mara baada ya kurejea kwa umeme," amesema Dkt. huyo.
Wakazi wa Tungi wametoa wito kwa jamii kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu na kuhakikisha taarifa wanazosambaza ni sahihi ili kuepuka kuharibu juhudi nzuri za maendeleo zinazofanywa kwa ajili ya wananchi.
No comments:
Post a Comment