Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Vyama vya Siasa kuhusu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika leo Julai 27, 2025 jijini Dodoma na kushirikisha vyama vyote vyenye usajili kamili.
Na. Mwandishi Wetu.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewahakikishia viongozi wa vyama vya siasa kuwa kutakuwa na uwanja sawa kwa vyama vyote wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuhakikisha kila chama kinafanya mikutano yake kwa mujibu wa ratiba.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele ameyasema hayo leo tarehe 27 Julai, 2025 wakati akifungua mkutano wa Tume na Viongozi wa Vyama vya Siasa jijini Dodoma.
”Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, inawahakikishia kuwepo kwa uwanja sawa kwa vyama vyote wakati wa kampeni kwa kuhakikisha kila chama kitafanya mikutano yake kwa mujibu wa ratiba itakayokuwa imepitishwa na kamati ya ratiba ngazi ya Taifa inayoratibu ratiba ya kampeni ya wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais, kamati ya jimbo inayoratibu ratiba ya wagombea wa ubunge na kamati ya kata inayoratibu ratiba ya wagombe wa udiwani,” amesema Jaji Mwambegele.
Amewasisitiza viongozi hao wa vyama vya siasa kuwasihi wagombea na wafuasi wao kufanya kampeni za kistaarabu na kuepuka kufanya vitendo vitakavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi.
”Kipindi cha kampeni kunakuwa na joto kali la kisiasa linalotokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu wa kisiasa hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi,” amesema.
Jaji Mwambegele amewahakikishia viongozi hao wa vyama kuwa katika kipindi cha utoaji fomu za wagombea ambacho kinaanza tarehe 09 Agosti, 2025 hadi tarehe 27 Agosti, 2025 kwa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais na tarehe 14 Agosti, 2025 hadi tarehe 27 Agosti, 2025 kwa wagombea wa Ubunge na Udiwani, Tume itazingatia sheria.
” Tume inapenda kuwahakikishia kwamba, katika kipindi cha utoaji wa fomu za uteuzi na siku ya uteuzi wa wagombea, tutasimamia Katiba, Sheria na Kanuni ili kuhakikisha kila mwenye sifa ya kugombea anapata haki ya kupewa fomu na kuteuliwa pale atakapotimiza masharti ya uteuzi,” amesema.
Viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa wakishiriki mjadala.
No comments:
Post a Comment