HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 22, 2025

RAIS DKT. SAMIA KUZINDUA BANDARI KAVU YA KWALA NA KONGANI YA VIWANDA MKOANI PWANI

 


Na Khadija Kalili – Michuzi TV
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya ziara ya siku moja mkoani Pwani mnamo Julai 31, 2025 kwa ajili ya kuzindua rasmi Bandari Kavu ya Kwala pamoja na Kongani ya Viwanda iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini, Mkoa wa Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Kibaha leo Julai 22, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakari Kunenge, amesema kuwa maandalizi ya mapokezi ya Mhe. Rais yamekamilika, na kwamba ziara hiyo ni ya kihistoria kwa mkoa huo kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika eneo la Kwala.

“Rais Dkt. Samia atazindua Bandari Kavu ya Kwala, eneo ambalo serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda zaidi ya 250 katika Kongani ya Viwanda ya Kwala, ambayo ni miongoni mwa kongani kubwa zaidi nchini,” amesema RC Kunenge.

Mbali na uzinduzi wa bandari kavu na kongani ya viwanda, Mhe. Rais Samia pia atazindua rasmi safari za treni ya kisasa ya mwendokasi (SGR) kwa ajili ya kubeba makasha kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma.

Kwa mujibu wa Kunenge, Bandari Kavu ya Kwala ina uwezo wa kuhudumia makasha 823 kwa siku na takribani makasha 30,000 kwa mwaka.

“Bandari hii inalenga kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam kwa takribani asilimia 30 na kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi,” alifafanua.

Aidha, RC Kunenge amesema kuwa Rais Dkt. Samia pia atazindua maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari kavu kwa nchi jirani zisizo na bandari baharini ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia, Burundi, Malawi, Zimbabwe na Uganda. Ameongeza kuwa nchi za Sudan na Somalia pia zimeonyesha nia ya kuwekeza katika eneo hilo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais anatarajiwa kupokea mabehewa 160 ya reli ya kati, ambapo kati yake mabehewa 100 yamenunuliwa mapya na serikali, mabehewa 20 yamekarabatiwa, na mengine 40 yamekarabatiwa kwa ushirikiano na Shirika la Chakula Duniani (WFP) pamoja na Wakala wa Ushoroba wa Kati.

Rais Dkt. Samia pia ataweka jiwe la msingi kwenye Kongani ya Viwanda ya Kwala, yenye jumla ya viwanda 250, hatua inayolenga kuimarisha uchumi wa viwanda nchini na kuongeza ajira kwa Watanzania.

Kwa ujumla, ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Pwani inatarajiwa kuleta chachu ya maendeleo na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji wa kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad