HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 22, 2025

DKT. HUSSEIN OMAR AIPONGEZA TET KATIKA JITIHADA ZA KUKUZA SEKTA YA ELIMU NCHINI

-Avutiwa na Utendaji katika Mifumo ya TEHAMA

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Hussein Mohamed Omar ameipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa jitihada wanazofanya za kukuza Sekta ya Elimu nchini hasa kupitia eneo la mifumo ya TEHAMA inayosaidia katika ujifunzaji na ufundishaji.

Amesema hayo leo Julai 22, 2025 alipofanya ziara ya kujionea utendaji kazi wa taasisi iliyopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam, na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Aneth Komba aliyeambatana na wajumbe wa menejimenti ya Taasisi ya Elimu Tanzania.

"Nimefurahishwa na utendaji kazi wa Taasisi ya Elimu hasa kwenye eneo la mifumo ya TEHAMA ambayo inasaidia kuwafikia walimu takribani nchi nzima," amesema Dkt. Hussein Omar.

Sambamba na hilo, amepongeza Mitaala iliyoboreshwa kwa namna inavyoenda kuwa suluhu katika kukabiliana dhidi ya changamoto ya ajira nchini hasa kwa kundi kubwa la vijana, kwani kupitia mkondo wa Amali Mtaala unaotoa fursa kwa mwanafunzi kuchagua fani anayopenda kuisomea pindi amalizapo darasa la sita.

Aidha, Dkt. Hussein Omar ametoa wito kwa TET kuandaa Mtaala utaosaidia kukabiliana na changamoto ya taka ngumu ambayo husumbua hasa katika majiji makubwa nchini, yakiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mwanza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba amesema Taasisi ya Elimu Tanzania ipo tayari kutekeleza maelekezo kutoka kwa Dkt. Hussein Mohamed Omar hasa katika kufanya utafiti kwenye maeneo ambayo hayana vifaa vya TEHAMA lakini yana uhaba wa walimu ili kuyapa kipaumbele maeneo hayo katika awamu inayokuja.

Sambamba na hilo amesema kupitia kitengo cha Utafiti TET imepokea maelekezo ya kuona namna ambavyo Mtaala ulioboreshwa kupitia Elimu ya Amali ilivyoleta mabadiliko katika Sekta ya Elimu nchini.











No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad