HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 9, 2025

PURA YATAMBA KUONGEZA USHIRIKI WA WATANZANIA KATIKA SHUGHULI ZA MAFUTA NA GESI

 



Na Karama Kenyunko
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imetangaza mafanikio makubwa katika kuimarisha ushiriki wa Watanzania kwenye sekta ya mafuta na gesi, ambapo kiwango cha ushiriki wa kampuni za ndani kimeongezeka hadi kufikia asilimia 85.

Akizungumza leo Julai 9, 2025, katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam ambako yanaendelea Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, amesema kuwa ongezeko hilo ni matokeo ya jitihada za makusudi za kuhakikisha Watanzania wanahusishwa moja kwa moja katika shughuli za utafiti na uchimbaji.

Amesema kuwa awali, mwaka 2018, wakati kampeni ya awali ya uchimbaji ilipoanza katika maeneo ya baharini, kulikuwepo na meli maalum iliyofanya uchimbaji huo ikiwa na wafanyakazi 150, ambapo Watanzania walikuwa 52 – hatua aliyosema iliwapa nafasi nzuri ya kupata uzoefu wa moja kwa moja katika sekta hiyo.

“Zamani nafasi nyingi zilikuwa zinashikiliwa na wageni, lakini kwa sasa Watanzania wanapewa kipaumbele, jambo linalosaidia kuongeza ujuzi wa ndani,” alisema Mhandisi Sangweni.

Ameeleza kuwa kwa sasa kuna kampeni inayoendelea mkoani Mtwara ya kuchimba visima vitatu, huku PURA ikisisitiza matumizi ya kampuni za ndani kwa kazi zote zinazowezekana kufanywa na Watanzania.

Mhandisi Sangweni pia amepongeza jitihada za serikali kuwekeza kwenye elimu ya mafuta na gesi kupitia vyuo vikuu mbalimbali, akibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kukuza idadi ya wataalamu wa ndani wanaoweza kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.

Akizungumzia mwitikio wa wananchi katika maonesho ya Sabasaba, alisema kumekuwa na ongezeko la watu wanaotembelea banda la PURA, hali inayoashiria kuwa jamii inaendelea kuwa na mwamko na uelewa kuhusu rasilimali za mafuta na gesi.

“Wananchi wengi wanaonesha hamu ya kufahamu zaidi kuhusu sekta hii, na wamekuwa wakitoa maswali ya msingi kabisa,” aliongeza.

Kadhalika, alieleza kuwa suala la matumizi ya nishati safi ya kupikia limepewa kipaumbele kikubwa na serikali, akimtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa kinara katika kusukuma mbele ajenda hiyo, si tu ndani ya nchi bali hata katika ngazi ya bara na kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad