HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, July 5, 2025

Operesheni za Kukomesha Dawa za Kulevya Zaendelea Kwa Kasi Nchini

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeshiriki katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Saba Saba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya pamoja na sheria zinazohusu matumizi, usambazaji na uzalishaji wake.

Kamishna wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema kuwa ushiriki wa mamlaka hiyo katika maonesho haya ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha jamii juu ya athari za dawa za kulevya na kuelimisha kuhusu hatua za kisheria dhidi ya wahusika.

“Tupo hapa ili wananchi wapate elimu ya kutosha kuhusu dawa za kulevya — aina zake, madhara yake, na wajue kwamba sheria iko wazi kuhusu mtu yeyote atakayekamatwa akiwa anazimiliki, kuzisambaza au kuzitumia,” alisema Kamishna Lyimo.

Kwa mujibu wa Kamishna, DCEA inaendesha oparesheni maalum katika shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kutoa elimu ya kinga kwa vijana dhidi ya matumizi ya dawa hizo.

Wakati huo huo, mamlaka inaendelea na kampeni za kuwakamata wahusika wa biashara ya dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni juhudi za kuutokomeza kabisa mtandao wa usambazaji wa dawa hizo haramu.

Kamishna Lyimo pia alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita inaendelea kutoa huduma za matibabu bure kwa waathirika wa dawa za kulevya, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha kurejea katika maisha ya kawaida na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.

“Tunataka kila Mtanzania awe na afya njema na asiwe mateka wa uraibu wa dawa hizi hatari,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa DCEA, hali ya matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya imeendelea kuimarika kutokana na juhudi za mamlaka, huku dawa hatari kama heroin na cocaine zikionekana kupungua kwa kiasi kikubwa nchini.

Maonesho ya Saba Saba yataendelea hadi Julai 13, 2025, na DCEA inatoa wito kwa wananchi kutembelea banda lao ili kupata elimu ya kina na kushiriki katika mapambano dhidi ya janga la dawa za kulevya.









No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad