Bodi
ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) leo Julai 25, 2025,
wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitano kuanzia
tarehe 25 Julai 2025 hadi 24 Julai 2030.
Makubaliano
hayo ni muendelezo wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi hizo
mbili ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha wataalamu wa
kodi, wanachama, wanataaluma, wanafunzi na wadau wa taaluma ya uhasibu
na ukaguzi, pamoja na wapenda maendeleo wengine, kuhusu umuhimu wa
ukusanyaji wa kodi kwa maendeleo ya Taifa, usimamizi bora wa kodi,
viwango vya uandaaji wa hesabu na mbinu bora za ukaguzi wa hesabu.
Hafla
ya utiaji saini imefanyika Makao Makuu ya TRA jijini Dar es Salaam na
kuhusisha viongozi wakuu wa taasisi hizo. Hati hiyo imesainiwa na
Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusuph Juma Mwenda na Mkurugenzi Mtendaji wa
NBAA, CPA Pius Maneno.
Akizungumza
katika hafla hiyo, CPA Yusuph Juma Mwenda alieleza kuwa ushirikiano huu
utaimarisha zaidi ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa kuunganisha
nguvu na maarifa ya wataalamu wa taaluma ya uhasibu na ukaguzi nchini.
Alisisitiza kuwa TRA itaendelea kushirikiana kwa karibu na NBAA ili
kuhakikisha kwamba taarifa za kifedha zinazingatia viwango sahihi vya
kitaalamu, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi na uwazi katika masuala
ya kikodi.
Naye
CPA Pius Maneno, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, alisema kuwa makubaliano
hayo yamekuja katika wakati muafaka ambapo taasisi hiyo imezindua mfumo
mpya wa kiteknolojia uitwao NBAAVN, ambao utasaidia kutambua taarifa
halali za hesabu kwa kuwapatia namba maalumu ya utambuzi, hivyo
kukomesha matumizi ya wahasibu vishoka. Aliongeza kuwa mfumo huo
utarahisisha usomaji wa taarifa kati ya NBAA na TRA, hatua ambayo ni
muhimu katika kuhakikisha ufanisi wa pamoja.
Makubaliano
hayo yana nafasi ya kuendelezwa au kuongezewa muda pindi yatakapofikia
ukomo. Hatua hii ni mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine za umma, kwa
kuwa inaonyesha namna ambavyo ushirikiano wa karibu unaweza kuongeza
tija katika utoaji wa huduma na kuleta matokeo chanya katika maendeleo
ya Taifa.
Itakumbukwa
kuwa hii ni hati ya pili ya makubaliano kusainiwa na NBAA ndani ya
mwaka huu, baada ya ile ya tarehe 16 Mei 2025 kati ya NBAA na Taasisi ya
Wahasibu, Wakaguzi na Washauri wa Kodi Zanzibar (ZIAAT), ambayo pia
inalenga kuendeleza taaluma ya uhasibu na ushauri wa kodi nchini.
Makubaliano
hayo pia ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu umuhimu wa
taasisi za umma kushirikiana kwa karibu, kubadilishana taarifa na
kutumia teknolojia katika kuongeza uwazi, ufanisi na mapato ya Taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno (kushoto) pamoja na Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusuph Juma Mwenda (kulia) wakionesha hati ya makubaliano ya ushirikiano mara
baada ya kusaini makubaliano ya upatikanaji wa taarifa mbalimbali
zikiwemo za kikodi na kihesabu ikiwa sambamba na kusomana kwa mifumo
kati ya taasisi hizo mbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno (kushoto) pamoja na Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusuph Juma Mwenda (kulia) wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano ya
upatikanaji wa taarifa mbalimbali zikiwemo za kikodi na kihesabu ikiwa
sambamba na kusomana kwa mifumo kati ya taasisi hizo mbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno (kushoto) pamoja na Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusuph Juma Mwenda (kulia) wakibadilishana hati ya makubaliano ya ushirikiano mara baada ya kusaini makubaliano hayo katika ofisi za TRA Makao Makuu jijini Dar es Salaam
Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusuph Juma Mwenda akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa upatikanaji
wa taarifa mbalimbali zikiwemo za kikodi na kihesabu ikiwa sambamba na
kusomana kwa mifumo kati ya taasisi hizo mbili.
Mkutano ukiendelea
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno pamoja na Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusuph Juma Mwenda wakiwa
kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa NBAA na TRA mara
baada ya kusaini hati ya makubaliano ya upatikaji wa taarifa mbalimbali
kati ya taasisi hizo mbili
No comments:
Post a Comment