Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Elimu, Dkt. Hussein Omar akizungumza na Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda akizungumza na Menejimenti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), kujielimisha kuhusu shughuli zinazotekelezwa na Baraza hilo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Elimu, Dkt. Hussein Omar akizungumza na Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda wakati Naibu Katibu Mkuu alipofanya ziara Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), kujielimisha kuhusu shughuli zinazotekelezwa na Baraza hilo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Elimu, Dkt. Hussein Mohamed Omar, leo tarehe 21 Julai, 2025 amefanya ziara Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), kujielimisha kuhusu shughuli zinazotekelezwa na Baraza hilo.
Akiwa katika ofisi za NACTVET Kanda ya Mashariki jijini Dar es Salaam, Dkt Omar amepokea kwa Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda, taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya NACTVET.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt.Omar ameitaka NACTVET kuratibu uanzishaji wa miradi mbalimbali atamizi (incubator projects) ya kulea wahitimu wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuwawezesha kufanya kazi za uzalishaji wa bidhaa pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali pindi wanapohitimu.
“Naamini mnayo nafasi nzuri ya kuanzisha miradi tofauti kwa ajili ya kulea vijana wanaohitimu kutoka vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, pamoja na wale wanaotoka katika shule za sekondari zenye mkondo wa amali,” amesisitiza.
Aidha, Dkt. Omar amebainisha kwamba hatua hiyo itakuwa chachu ya kuwaongezea uwezo wahitimu hao kufanya ubunifu zaidi na kutekeleza shughuli za kiuchumi, ili kuwawezesha kuingia kwenye soko la ajira, na kutoa hamasa kwa vijana wengine kujipatia ujuzi.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda amesema Baraza kwa sasa linasimamia na kurekebu utoaji mafunzo katika jumla ya vyuo na taasisi 1,582 ikiwemo vyuo vya elimu ya ufundi 527, vyuo vya ufundi stadi 898, vyuo vya maendeleo ya wananchi 55 na Shule za Sekondari 102 zinazofundisha mkondo wa amali.
Dkt. Lingwanda amebainisha kuwa NACTVET imebuni mikakati mbalimbali kuimarisha ubora wa mafunzo, ikiwemo ya kuandaa na kuhuisha miongozo mbalimbali ya urekebu, kutengeneza mfumo endelevu wa ufuatiliaji ubora (Continuous Quality Improvement) pamoja na kuzisaidia taasisi zitoazo mafunzo kushirikiana na waajiri katika maboresho ya mitaala na kuhakikisha wahitimu wanakubalika katika soko la ajira.
Ziara ya Dkt. Omar ni mwendelezo wa ziara zake kwenye taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo tarehe 23 Juni, 2025, kumwezesha kujifunza na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo.
No comments:
Post a Comment