
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi, Wakili Patrick Kipangula (kushoto) akimkabidhi Press Card kwa Mtangazaji Mwandamizi wa Kituo cha Radio cha Wasafi Media, Diva Gisele Malinzi.
Na Mwandishi Wetu.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari -JAB, imempa onyo Mwandishi na Mtangazaji Mwandamizi wa Kituo cha Radio cha Wasafi Media, Diva Gisele Malinzi kwa kosa la kutangaza maudhui yanayokiuka maadili ya taaluma ya Habari na utangazaji ikiwa ni pamoja na kulazimisha kutoa taarifa binafsi za Msanii wa Muziki Ruta Maximilian Bushoke katika kipindi chake cha Lavidavi kilichorushwa hewani tarehe 07 Julai, 2025 kuanzia saa 4:00 hadi saa 6:00 Usiku.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 16 Julai, 2025, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi, Wakili Patrick Kipangula, amesema JAB imefikia uamuzi huo baada ya Kupokea Malalamiko kuhusu kipindi hicho, maudhui yake, maadili ya utangazaji na mwenendo wa uendeshaji wa kipindi ambacho Diva ni Mtangazaji wake.
Wakili Kipangula amesema Bodi ilimuita Mtangazaji huyo na kuzungumza naye Julai 14, 2025 na baada ya majadiliano na mashauriano ya muda Bodi ilibaini kuwa Mtangazaji Diva alikiuka maadili katika kipindi hicho na kumuonya kutokufanya makosa kama aliyoyafanya katika kipindi hicho.
Kwa upande wake, Diva alikiri kukosea na kuahidi kutorudia na kwamba anaishukuru Bodi kwa kubeba jukumu la ulezi, kuzungumza naye na kumuelekeza miiko ya taaluma na umuhimu wa kuzingatia maadili.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, inawakumbusha waandishi wa Habari, Wahariri, watangazaji, wapiga picha, na waandaaji wa maudhui ya kihabari kuzingatia maadili wakati wote wa utendaji kazi wao.
Bodi hii iliyoanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 11 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 5 ya Mwaka 2023, ni chombo cha kisheria ambacho chini ya kifungu cha 13 (a) cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 pamoja na majukumu mengine imepewa jukumu la kutoa Ithibati na Vitambulisho kwa Waandishi wa habari waliokidhi vigezo, kulea na kusimamia uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Pamoja na onyo hilo kwa Diva, Bodi pia imemkabidhi Mtangazaji huyo Kitambulisho chake cha Uandishi wa Habari (Presscards) baada ya kukidhi vigezo na kumtaka kuzingatia maadili ya taaluma na weledi katika utendaji kazi.
No comments:
Post a Comment