HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, July 26, 2025

EMEDO Yatoa Elimu ya Usalama wa Maji kwa Watoto Kawe

 

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
KATIKA kuadhimisha Siku ya Kuzuia Kuzama Maji Duniani, Shirika la EMEDO kwa kushirikiana na mradi wake wa Lake Victoria Drowning Prevention Project (LVDPP) limefanya kampeni ya utoaji elimu kwa wanafunzi katika Shule ya Msingi Ukwamani jijini Dar es Salaam, likisisitiza umuhimu wa elimu ya kujiokoa na hatua za tahadhari dhidi ya majanga ya maji.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mary Francis, Afisa Uchechemzi kutoka EMEDO na Mratibu wa Shirika la Kuzuia Kuzama Maji Tanzania, amesema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ni “Stori yako inaweza kuokoa maisha.” Amefafanua kuwa kushirikishana simulizi za uzoefu binafsi kuhusu majanga ya maji kunaweza kusaidia watu wengine kujifunza mbinu za kujikinga.

"Kwa wananchi wa Tanzania na hata nje ya mipaka yetu, wito wangu ni kujifunza kuogelea, kuwakinga watoto dhidi ya vyanzo vya maji wakiwa peke yao, na kuvaa makoti ya kuokoa maisha (life jackets) pindi unaposafiri majini,” amesema Mary.

Ameongeza kuwa takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa watu takribani 300,000 hufariki kila mwaka kwa kuzama maji, ambapo asilimia 90 ya vifo hivyo hutokea katika nchi za uchumi wa kati na zinazoendelea, huku watoto wenye umri wa miaka 1 hadi 15 wakiwa hatarini zaidi, hasa katika Bara la Asia.
Kwa upande wake, Helen Lucas Gasper, Afisa Jinsia na Ulinzi kutoka EMEDO, amesema shirika hilo linawapa kipaumbele watoto kwa kuwa ni rahisi kuwajengea uelewa wa awali kuhusu hatari za maji.

“Tumeanzisha klabu za wanafunzi mashuleni ili kufundisha ujumbe wa usalama wa maji. Ni muhimu kuifikia jamii kupitia watoto ambao wanaonyesha udadisi na uelewa wa haraka. Kawe tumeichagua kwa sababu ya ukaribu wake na Bahari ya Hindi,” alisema Helen.

Katika tukio hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ukwamani, Regina Cyrillo, alikiri kuwa kuna changamoto kubwa ya watoto kutoroka shule na kuelekea baharini, hasa kutokana na mazingira ya jamii yao kuwa karibu na fukwe. Amesema kuwa baadhi ya watoto hushawishika na matendo yasiyofaa kama vile kuogelea bila uangalizi na hata matumizi ya dawa za kulevya.

“Kuna watoto wa darasa la saba waliowahi kusumbua sana kutokana na kutoroka shule kwenda baharini. Wengine walijikuta kwenye matatizo kwa kuiga tabia hizo. Kwa sasa elimu imewasaidia na tunashukuru ushirikiano wa jamii na askari wa kata katika kuwathibiti,” amesema.

Aidha, alitoa wito kwa wazazi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha watoto wanapata lishe bora, akibainisha kuwa utapiamlo unaweza kuathiri maendeleo ya watoto kitaaluma na kimwili.

“Watoto wenye utapiamlo huwa na uelewa mdogo darasani. Tunahamasisha wazazi kuchangia mlo mashuleni na kuzingatia usalama wa watoto hususan wale wanaoishi karibu na fukwe maarufu kama Kawe Beach na Mbezi Beach,” alisema.


Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Kawe, Husna Nondo, amewashukuru EMEDO kwa kutoa elimu juu ya kuzuia kuzama kwa maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo baharini, madimbwi na sehemu zingine.

Amesema wamepata elimu juu ya matumizi ya lishe bora kwa watoto ili kusaidia kuondoa udumavu kwa watoto.

"Watoto wanapokosa lishe bora husababisha kuwa na uelewa mdogo darasani na kusababisha taaluma kushuka, hivyo kata na Wilaya yetu ya Kinondoni haitafanya vizuri. Hivyo basi kupitia hadhara hii nashauri wazazi kuweka kipaumbele juu ya suala zima la lishe bora kwa watoto na sisi kama viongozi tumeweza kusimamia katika ngazi zote za awali, msingi na sekondari ili kuhakikisha wanapata chakula wanapokuwa mashuleni," amesema.

Ameongeza, "tunasisitiza wazazi kuendelea kuchangia na kuwawezesha watoto waendelee kupata mlo kamili shuleni na kuimarisha afya ya akili kupitia lishe bora."

Amesema wazazi watambue kuwa katika kata hiyo kuna Bahari maarufu kama fukwe za Kawe na Mbezi, hivyo ni muhimu kuzingatia suala la usalama wa watoto katika maeneo yao ili kuepukana na vifo vya maji.

"Kuna baadhi ya watoto wanatoroka shuleni na majumbani kwa wazazi kwenda kwenye fukwe hizi. Nikumbushe tu, baharini si sehemu ya kucheza watoto. Hivyo kupitia mkutano huu natoa wito kwa watoto kutokwenda baharini bila uangalizi wa wazazi, walezi au walimu. Kwa kuzingatia hayo, vifo vya maji vitazuiwa," amesema.

Shirika la EMEDO limesisitiza kuwa elimu ya kujiokoa majini inapaswa kuwa sehemu ya mitaala ya masomo kama Physical Education (PE) na vipindi vya ziada (extra-curricular), hata kama ni kwa njia ya nadharia kutokana na changamoto ya mazingira yasiyoruhusu mafunzo ya vitendo.

Kwa ujumla, maadhimisho haya yamelenga kuhamasisha hatua za kinga na uokoaji, kwa lengo la kupunguza vifo vinavyotokana na kuzama maji, hasa kwa watoto na wavuvi walio katika hatari zaidi.







No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad