Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaa, Mheshimiwa Albert Chalamila ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kuwaelimisha wajasiriamali wa mtandaoni kuhusu fursa zilizopo na namna wanavyoweza kushirikiana na taasisi hii kubwa zaidi ya fedha nchini kujikwamua kiuchumi.
Pongeza hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki kwenye Semina ya Instaprenyua iliyowakutanisha wajasiriamali na waelimishaji wa mada tofauti kuhusiana na jinsi wanavyoweza kukuza biashara zao na kujiongezea kipato.
Akizungumza na wajasiriamali hao, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwe Makwiro aliyemwakilisha Mheshimiwa Chalamila amesema kinachofanywa na benki ya CRDB kuwajengea uwezo wajasiriamali kinaunga mkono jitihada za serikali inayojitahidi uweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini kukuza kipato chao.
“Maarifa ya kufanya biashara ni nyenzo muhimu ya mafanikio katika biashara pengine kuliko hata mtaji fedha. Mafunzo haya yanayotolewa na Benki ya CRDB yanafungua fursa ambazo mjasiriamali hakuwa anazifahamu. Nawapongeza sana Benki ya CRDB kwa kutenga muda wa kukaa na wajasiriamali hawa na kuwaonyesha namna ya kushirikiana nanyi kukuza biashara zao,” amesema Charangwe.
Kukua kwa sayansi na teknolojia kumerahisisha mambo mengi duniani katika karne hii ya 21 ikiwamo namna ya kufanya biashara kwani sasa hivi kwani mfanyabiashara anaweza kumuuzia mteja ambaye haaonani na kila kitu kikaenda vizuri.
Charangwe amesema Serikali imeweka juhudi kubwa kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa zilizopo kwenye mitandao ya kijamii kwa kuweka mazingira rafiki ya kumiliki simu za kisasa, upatikanaji wa intaneti pamoja na ulinzi wa taarifa za watumiaji wa mitandao ya kijamii.
“Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha mpaka Juni 2025 tulikuwa na jumla ya laini milioni 92.7 za simu zilizosajiliwa na kati ya hizi, zaidi ya laini milioni 54.1 zilikuwa zinatumia intaneti. Idadi ya watu waliofikiwa na huduma za intaneti ni asilimia 93. Ongezeko la matumizi ya intaneti nchini linatokana na kukua kwa mahitaji. Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara ikiwamo kujenga miundombinu ya mawasiliano,” amesema Makwiro.
Akieleza kuhusu mikakati ya kuwawezesha wajasiriamali nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema Semina ya Instaprenyua ni jukwaa mahsusi la kujadili teknolojia mpya, mbinu bunifu za masoko, ulinzi wa kidijitali, na jinsi wajasiriamali wa mtandaoni wanavyoweza kunufaika na mikopo nafuu kutoka benki ya CRDB.
“Katika dunia ya leo ya karne ya 21, biashara si suala la mahali tena bali namna gani muuzaji anaweza kumfikia mteja. Hii ndiyo sababu Benki ya CRDB tumeendelea kuipa umuhimu mkubwa semina hii ya Instaprenyua tangu tulipoizindua mwaka 2022 tukitambua kwamba katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la matumizi ya teknolojia katika kuendesha biashara, jambo kubwa ambalo mjasiriamali wa kisasa hawezi kulikwepa,” amesema Nsekela.
Benki ya CRDB, amesema inamrahisishia mfanyabiashara kukusanya malipo anayoyapokea kupitia huduma ya LIPA HAPA kutoka kwa mteja hata aliye mbali naye huku ikimruhusu mteja kulipia bidhaa au huduma azitakazo SimBanking, mitandao ya simu, au TemboCard. Mifumo hii yote amesisitiza kuwa ni ya haraka, ina usalama na ufanisi mkubwa na ndiyo msingi wa biashara ya kidijitali yenye mafanikio.
Kuhusu upatikanaji wa mitaji, Nsekela amesema “Benki ya CRDB imekuwa kinara katika uwezeshaji wa wajasiriamali kupitia Akaunti ya Hodari ambayo ni kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na Akaunti ya Biashara kwa wajasiriamali wa kati.
Akaunti hizi huwaunganisha wajasiriamali na fursa za mikopo ya uwekezaji na mikopo ya uendeshaji ikiwamo ‘Komboa loan’ mahsusi kwa wafanyabiashara wanaoagiza mizigo kutoka nje ya nchi. Vilevile tunatoa mitaji wezeshi kupitia Taasisi yetu ya CRDB Bank Foundation ambapo wafanyabiashara wachanga hupewa kwanza kabla hawajapewa mitaji wezeshi kukuza biashara zao.”
No comments:
Post a Comment