HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 20, 2025

WAJUMBE WANNE BARAZA LA KATA MSITU WA TEMBO SIMANJIRO KORTINI KWA RUSHWA

 


Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WAJUMBE wanne wa baraza la ardhi la kata ya Msitu wa Tembo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh120,000.

Wajumbe hao wamefikishwa kwenye mahakama ya wilaya ya Simanjiro wakisomewa shtaka la kuomba na kupokea rushwa hiyo ili kutoa upendeleo kwenye shauri.

Katika shauri hilo la jinai namba 14400/2025 limesomwa mji mdogo wa Orkesumet mbele ya hakimu mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Simanjiro Onesmo Nicodemo.

Washtakiwa hao wanne ambao ni wajumbe wa baraza la ardhi la kata ya Msitu wa Tembo ni Elias Kimweri, Felister Mphuru, Ally Mphuru na Joseph Simbeye wakazi wa kijiji cha Msitu wa Tembo.

Mwendesha mashtaka wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) Faustin Mushi akisoma hati ya mashtaka amesema washtakiwa hao wametenda kosa hilo mwezi Mei mwaka 2025.

Mushi amesema washtakiwa hao kwa kushirikiana walimshawishi kwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh120,000 kwa Issa Njuju.

Amesema washtakiwa hao kwa pamoja waliomba na kuchukua hongo hiyo ili kumsaidia Njuju kushinda shauri la ardhi lililokuwa limefunguliwa katika baraza hilo dhidi yake.

Amesema washtakiwa hao wametenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) na 15 (2) vya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sura ya 329 R.E.2022.

Hata hivyo, Hakimu Nicodemo alipowauliza washtakiwa hao wanne kama ni kweli wametenda kosa hilo wamekana shtaka hilo.

Hakimu Nicodemo ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 25 mwaka 2025 itakaposikilizwa hoja ya awali (PH).

Washtakiwa hao wanne wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya bondi katika kesi hiyo

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad