Na Mwandishi Wetu – Dodoma 04 Juni 2025
Mamia ya wananchi wamejitokeza katika banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupata huduma mbalimbali za kielimu na kiafya wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yanayoendelea jijini Dodoma.
Miongoni mwa vivutio vikubwa katika banda hilo lililoko viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), ni huduma ya tiba ya kuimarisha kinga ya mwili kwa kutumia nyuki (api-therapy), iliyokuwa ikitolewa na Mhifadhi Brenda Mwakipesile kutoka TFS.
Mwakipesile alisema tiba hiyo ya asili inasaidia kuchochea kinga ya mwili na kutoa ahueni kwa baadhi ya maumivu ya muda mrefu, hasa ya viungo.
“Tiba hii inatumia sumu ya nyuki kwa njia salama na inayodhibitiwa, na imekuwa na matokeo chanya kwa baadhi ya wagonjwa waliowahi kuipokea. Leo tumeona muitikio mkubwa wa wananchi walio na shauku ya kujifunza na kupata huduma hii,” alisema.
Mbali na huduma hiyo, TFS ilitoa elimu kwa wananchi kuhusu uhifadhi wa misitu, matumizi ya nishati safi ya kupikia, uzalishaji wa mkaa mbadala, upandaji wa miti na utunzaji wa vyanzo vya maji.
Maonesho haya yamebeba kaulimbiu: “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa – Dhibiti Matumizi ya Plastiki”, yakihusisha taasisi mbalimbali za Serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na wananchi.

“Nimejifunza mengi kuhusu misitu, lakini pia sikuwahi kufikiria nyuki wanaweza kutumika kama tiba. Ni jambo jipya na la kuvutia sana,” alisema Rehema John, mkazi wa Dodoma.
Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira yanatarajiwa kufikia kilele chake Juni 5, yakilenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa mustakabali wa Taifa.
No comments:
Post a Comment