HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 25, 2025

TANZANIA YATHIBITISHA DHAMIRA YAKE YA KUIMARISHA SEKTA YA POSTA AFRIKA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholaus Merinyo Mkapa amethibitisha dhamira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuunga mkono shughuli za Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na kueleza kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama katika kuboresha mifumo ya Mawasiliano, kukuza uchumi wa kidijitali na kuhakikisha huduma za Posta zinabaki kuwa kiungo muhimu kwa jamii.  

Bw. Mkapa ameeleza hayo tarehe 24 Juni, 2025 wakati akifungua mkutano wa 43 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU), unaofanyika katika Jengo la PAPU, jijini Arusha na kuhudhuriwa na nchi wanachama takribani 45 pamoja na wadau, mashirika na Taasisi mbalimbali za Kimataifa.

Aidha,  Bw. Mkapa akizungumza katika ufunguzi huo amewasisitiza washiriki kutumia kikao hicho kama jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika mageuzi ya sekta ya Posta barani Afrika kwa kuongeza ubunifu na kutumia teknolojia ili kuiwezesha sekta ya Posta kuendelea kustawi na kutoa huduma bora zinazoendana na mahitaji ya wateja katika kupata huduma za Posta na Mawasiliano.

Katika hatua nyingine,  Bw. Mkapa amepongeza juhudi za PAPU katika kuongoza mwelekeo mpya wa huduma za Posta Afrika, sambamba na kupongeza kamati za ufundi kwa maandalizi na mapendekezo madhubuti yaliyowasilishwa katika mkutano huo yenye lengo la kuboresha sekta ya posta Afrika.

Kwa upande wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bi. Cecilia Mkoba ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TCRA ameeleza kuwa ili Sekta ya Posta ikidhi mahitaji halisi ya maisha ya watu inatakiwa kuendana na maendeleo ya Teknolojia sambamba na kutumia mkutano huu kubadilishana uzoefu katika kuboresha Sekta ya posta Afrika.

Naye Katibu Mkuu Umoja wa Posta Afrika (PAPU) Bw. Chief Sifundo Moyo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mamlaka za Serikali za nchi wanachama Pamoja na Wakuu wa Taasisi kwa ushirikiano unaoendelea kutoa katika Sekta ya Posta barani Afrika.








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad