Mtuhumiwa James Mbapila, anayedaiwa kuchakachua mitungi ya gesi, akiwa chini ya ulinzi ofisini kwake, baada ya askari polisi kwa kushirikiana na Kampuni ya Orxy Energies, kufanya operesheni maalumu ya kuwakamata watuhumiwa, mtaa wa Libya, Dar es Salaam.
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA)kwa kushirikiana na Oryx Gas pamoja na Jeshi la Polisi wamefanya operesheni ya kukamata watu wanaofanya uchakachuaji wa wa gesi ya kupikia nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya Oryx Gas kufanya operesheni maeneo ya Kariakoo na Upanga na kufanikiwa kukamata watu wanaochakachua gesi, Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki Mhandisi Nyirabu Musira amesema hatua zinazochukuliwa na wadau wakiwemo wa Oryx Gas ni jambo jema na ni wajibu wa kampuni hizo kuhakikisha usalama wa mitungi pamoja na ujazo unaostahili.
"Nitoe mwito kwa kampuni za gesi ya kupikia kuendelea kushirikiana na EWURA kudhibiti mitungi yao ya gesi ambayo inauzani wa zaidi ya kilogramu 16 kwasababu mitungi hiyo ndio inayotumiwa mara nyingi kwa ajili ya uchakachuaji na kanuni iko wazi inasema ni wajibu wa kampuni kufuatilia mitungi hiyo.
"EWURA imekuwa ikishirikiana na Kampuni za nishati safi ya kupikia kufanya ukaguzi mara kwa mara na kwa wale ambao wamekuwa wakifanya biashara bila utaratibu na kufanya uchakachuaji wa gesi kwenye mitungi adhabu yake ni faini Sh.milioni 20 au kifungo cha miaka mitatu jela ama vyote kwa pamoja.
"Tumekuwa tukichukua hatua kwa wale ambao wanafanya biashara hiyo bila kufuata utaratibu na walichokifanya Oryx Gas pamoja na wadau wengine wa kampuni za gesi ni sehemu ya wajibu wao maana leseni ambazo tumewapa zinataka pia kulinda usalama wa mitungi pamoja na kuzingatia ujazo kulingana na uzito unatakiwa kwa mtungi husika."
Akieleza zaidi Mhandisi Musira amesema kanuni ya usimamizi wa LPG inazitaka Kampuni zinazoingiza na kusambaza gesi kuhakikisha wanaifuatilia kujua nani anamiliki na inafanyiwa biashara kwa namna gani huku akisisitiza kuwa biashara hiyo inakuwa katika mazingira yaliyo sahihi na salama .
Kwa upande wake Meneja Mauzo Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Shaban Fundi akizungumza kuhusu operesheni ya kukamata wanaochakachua gesi amesema wamekuwa wakifanya ukaguzi mara kwa mara na kutoa ombi kwa Serikali na taasisi zake kuongeza nguvu kuwadhibiti wanaofanya uchakachuaji huo.
“Tumekuwa tukifanya kazi kubwa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia lakini tunatamani kuona wananchi wanapata ujazo wa gesi ambao unaendana na uhalisia.Hatuko tayari na hatufurahishwi na watu ambao wanafanya uchakachuaji,hivyo tumekuwa tukifanya operesheni kama hizi kuwadhibiti watu hao.”
Amefafanua mtungi unapotumika vibaya au kujazwa kinyume cha taratibu unaweza kuhatarisha maisha ya watu na hiyo inaweza kurudisha nyuma nguvu nyingi zinazofanyika kati ya wao kama wawekezaji pamoja na Serikali katika kuhamasisha mafumizi ya nishato safi ya kupikia.
"Tumewakamata hawa watu ambao wamekuwa wakifanya uchakachuaji wa gesi na tutaendelea kufanya juhudi hizi lakini naendelea kusisitiza tunahitaji msaada wa taasisi kama EWURA,Wakala wa Vipimo na Polisi kuendelea kuongeza nguvu na kwa pamoja tukomeshe wanaofanya biashara hii kinyuma cha utaratibu na wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Amefafanua zaidi amesema kinachofanywa na watu hao kinawaathiri watumiaji kwasababu mitungi inakuwa haijai na pia wanafanya njia inayotumika kujaza gesi inakuwa si salama kwasababu mteja anaweza kutumia gesi na likatokea jambo lolote na hivyo kuleta madhara kwa mtumiaji.
"Wakati tunajaza mitungi ya gesi katika vituo vyetu tuna hatua mbalimbali ambazo tunazifuata za kuhakikisha usalama wa hali ya juu unazingatiwa, ila hawa watu wanapofanya wizi huu hawatumii vigezo vyovyote vya kuzingatia usalama…
“Kwahiyo lolote linaweza kutokea na sisi hatutaki lolote litokee, ndio maana tunafanya juhudi hizi kuzuia na tunatoa mwito sisi pekee yetu hatuwezi au kampuni hizi za gesi haziwezi kufanya operesheni peke yao.Tunahitaji nguvu ya pamoja na wanaokamatwa wachukuliwe hatua kali za kisheria.”

No comments:
Post a Comment