HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, May 18, 2025

WATAFITI SUA WAJA NA DAWA MPYA YA MITISHAMBA DHIDI YA HOMA YA KIWELE

 






WAFUGAJI mkoani Iringa wameonyesha mwitikio chanya wa kutumia dawa mpya ya mitishamba iliyobuniwa kwa ajili ya kutibu homa ya kiwele kwa mifugo, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama za matibabu na kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa.

Wakizungumza mara baada ya kupatiwa mafunzo kutoka kwa watalaam Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wafugaji wameelezea matumaini makubwa kwa tiba hiyo ambayo inatokana na mti dawa wa asili, ikiwa ni matokeo ya tafiti bunifu chini ya mradi wa NANO COM unaolenga kuboresha afya ya mifugo na kuinua kipato cha jamii za wafugaji.

"Kwa muda mrefu tumekuwa tukitumia dawa ghali zisizoendana na mazingira yetu. Hii dawa mpya ni ukombozi kwetu," alisema Kalekwa Abdala, mmoja wa wafugaji waliopokea mafunzo hayo.

Kwa upande wao Gabriel Fuime na Hawa Ally Mbata, walisisitiza kuwa matumizi ya mitishamba ni sehemu ya utamaduni wao, lakini walikuwa wakikosa uelewa wa kitaalamu. "Kupitia SUA sasa tunakwenda kupata tiba salama na bora, iliyotengenezwa kwa utaalamu wa kisayansi hapa hapa nchini," alisema Hawa.

Prof. Gaymary Bakari, Mhadhiri wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya kutoka SUA na Mkuu wa Mradi wa NANO COM, alisema dawa hiyo imeonesha mafanikio katika hatua za awali za tafiti na inalenga kuwa suluhisho rafiki, la gharama nafuu kwa wafugaji.

Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Kata ya Kitwiru, Peter Raymondi Sigunga, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha tafiti hizo kufanyika, akieleza kuwa zaidi ya asilimia 98 ya mifugo hukumbwa na homa ya kiwele.
"Jumla ya wafugaji 38 kutoka kata za Kitwiru na Mkimbizi wamepata mafunzo, wanawake wakiwa ni 18. Hii ni hatua kubwa kuelekea mapinduzi ya tiba ya mifugo," alisema.

Mradi wa NANO COM unatekelezwa kwa ushirikiano wa SUA na Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo ya Utafiti cha Canada (IDRC), ukiwa na lengo la kuimarisha afya ya wanyama, usalama wa chakula, lishe na kipato kupitia mnyororo wa thamani wa maziwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad