Wakandarasi waliopewa kazi za ujenzi wilayani ilala, Mkoani Dar es salaam, wametakiwa kuhakikisha hadi ifikapo mwezi juni mwaka huu wawe wamekamilisha miradi yote ya barabara kwa wakati.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika miradi ya maendeleo kwenye sekta ya miundombinu alipokagua barabara na madaraja.
Mpogolo amesema kuwa wakandarasi waliopewa kazi katika halmshauri ya jiji watumie muda uliobaki baada ya mvua kukatika kurudi katika miradi hiyo kuendelea na ujenzi ili wananchi waendelee kupata huduma baada ya miradi hiyo kusimama kutokana na mvua.
Mpogolo, amekagua miradi ya barabara yenye urefu kilometa 7 na madaraja zaidi ya matatu yanayojengwa kwa mapato ya ndani, katika jimbo la Segerea, Ilala na Ukonga.
Mkuu huyo wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amemshukuru Rais Dokta Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 10. 7 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za ndani zinazojengwa kwa kiwango cha lami pamoja na madaraja ili kurahisha mawasiliano kwa wananchi.
Amesema fedha hizo tayari zimeanza kujenga madaraja 3 katika jimbo la Ukonga na Segerea na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 7 ambazo zinajengwa katika maeneo ya liwiti, kariakoo na pugu halisi.
Mpogolo ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wabunge wote watatu wanaotoka katika halmashauri ya jiji la Ilala kwa jitihada kubwa walizofanya pamoja na baraza la madiwani kwa kuhakikisha bajeti ya mwaka huu inapitishwa ili kukamilisha miradi ya maendeleo.
Ambapo pia amewaomba wananchi kuendelea kuwa na subira kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa ujenzi wa miradi hiyo, na kuwahimiza wakandarasi kufanya kazi zao na kutimiza wajibu wao ili wakamilishe miradi hiyo.
Amesema wakandarasi ambao walikwama kutokana na mvua kushindwa kubeba malighafi kufika eneo la ujenzi sasa waanze kazi kutokana na mvua kuanza kupungua, na halmashauri itatumia vifaa vyake ili kukarabati barabara za pembezoni zirudi katika hali ya kawaida.
Mpogolo, amebainisha baraza la madiwani katika halmashauri ya jiji la Dar es salaam, kwa kushirikiana na mkurugenzi wa jiji Helihuruma Mabelya wanaendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuhakikisha wakandarasi wanalipwa fedha zao kwa wakati.
Aidha Mpogolo, amewataka tarura wilayani ilala, kuwachukulia hatua wakandarasi wasiomaliza kazi, wasumbufu na kulalamika bila kutimiza wajibu wao wasipewe kazi nyingine kwa kushindwa kutimiza wajubu wao.
Amesema wakandarasi wenye sifa na wanaofanya kazi zao vizuri katika miradi ndiyo wawe na sifa za kuendelea kufanya kazi ili fedha zinazotolewa ziendane na kazi zinazifanywa kwa kuleta tija kwa wananchi wenye changamoto ya miumdombinu katika maeneo yao.
Kuhusu wananchi waliojenga pembezoni mwa madaraja makubwa yanayopitisha maji mengi, Mpogolo amewasihi wananchi hao kuondoka na kuwapongeza wale ambao wamechukua hatua za kuhama baada ya kuona wapo katika mikondo ya maji hali inayohatarisha usalama wao.
Kwa upande wake Mwandisi Greyson Nzunda wa halmashauri ya wilaya ya Ilala, amemuhakikishia mkuu huyo wa wilaya, Tarura itahakikisha inawasimamia wakandarasi wanarudi katika maeneo ya miradi mara moja baada ya mvua zinazoendelea kukatika.
Amesema nia ya tarura ni kuhakikisha miundombinu yote iliyokua na changamoto inajengwa na kurudisha mawasiliano kwa wananchi kwa kata moja na nyingine.
Mzunda ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa fedha hivyo wananchi wategemee ukamilikaji wa miradi hiyo na wao kuendelea kupata huduma nzuri za kijamii ili waendelee kujiletea maendeleo.
Amesema kipindi hiki cha mvua miradi mingi ilisimama na wakandarasi wengi kushindwa kuendelea na kazi hivyo watahakikisha kazi zote zilizosimama zinaendelea baada ya mvua kukatika.
No comments:
Post a Comment