Dodoma, 2 Mei 2025 –MALAWI imetangaza rasmi kuondoa marufuku ya uagizaji wa mazao ya mimea kutoka Tanzania, hatua inayofungua ukurasa mpya katika uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo jirani.
Uamuzi huo umetangazwa wakati wa Mkutano wa Pamoja wa Mawaziri wa Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dodoma, ukiwaleta pamoja viongozi waandamizi wa sekta za Mambo ya Nje, Kilimo, Biashara na Habari kutoka pande zote mbili.
Hatua hiyo ya Malawi inafuatia majadiliano ya kina kufuatia agizo la Serikali ya Tanzania lililotolewa tarehe 13 Machi 2025, lililopiga marufuku uingizaji wa baadhi ya bidhaa kutoka nje – hatua iliyozua changamoto kwa biashara baina ya nchi hizo mbili.
Mkutano huu muhimu ni muendelezo wa mashauriano ya tarehe 24 Aprili 2025 kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mheshimiwa Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, na mwenzake wa Malawi, Mheshimiwa Dkt. Nancy Gladys Tembo.
Katika kujibu hatua hiyo ya Malawi, Tanzania ilikuwa imetoa marufuku ya muda mnamo 23 Aprili 2025 dhidi ya baadhi ya mazao kutoka Malawi. Hata hivyo, kutokana na majadiliano ya pamoja, pande zote zimekubaliana kufungua tena njia za biashara kwa kuheshimu miongozo ya kikanda na kimataifa kuhusu usafi, viwango na usalama wa mazingira.
Serikali ya Malawi, kwa upande wake, imeahidi kutoa mamlaka rasmi kuruhusu biashara huru ya bidhaa kuanzia tarehe ya taarifa hii, ikiwa ni dalili ya dhamira ya kweli ya kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kibiashara.
Aidha, nchi hizo zimekubaliana kukamilisha taratibu za kisheria za kuidhinisha Makubaliano ya Mfumo wa Biashara Uliorahisishwa ifikapo tarehe 30 Mei 2025.
Hii ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa maazimio ya kikao cha sita cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kilichofanyika Februari mwaka huu mjini Lilongwe.
Mkutano huo umehitimishwa kwa mafanikio, huku ujumbe wa Malawi ukitoa shukrani za dhati kwa Tanzania kwa ukarimu na maandalizi bora. Viongozi wa nchi zote mbili pia walipongezwa kwa mchango wao katika kudumisha uhusiano wa kihistoria na wa kirafiki kati ya mataifa hayo.
No comments:
Post a Comment