Na Mwandishi Wetu
WAFANYAKAZI 20 wa hoteli ya Lark iliyopo ndani ya jengo la Noble Centre Dar es Salaam, linalomolokiwa na CRJE wamezuiwa kuingia ndani ya hoteli hiyo kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni mgogoro wa kimkataba baina ya mwekezaji wa hoteli hiyo na wamiliki wa jengo.
Hatua hiyo imezua taharuki na vilio miongoni mwa wafanyakazi hao,huku wakilalamika kunyimwa haki zao bila taarifa rasmi kutoka kwa muajiri wao.
Mfanyakazi na kiongozi wa wafanyakazi wa hoteli hiyo, Irene Mushi amesema walifika kazini kama kawaida asubuhi wakiwa katika sare zao za kazi, lakini walishangazwa na hatua ya kuzuiwa kuingia ndani na walinzi wa jengo.
“Sisi tunatofautiana kuingia kazini wapo wa mchana na wengine usiku, lakini jana tulianza kuona dalili mbaya za milango ya baadhi ya sehemu kama vile vyumba vya wafanyakazi na vile vya kubadilishia nguo vimefungwa kwa kufuli. Mwezetu aliyeingia usiku alizuiwa kuingia jana jioni bila sababu. Tulipojaribu kuwasiliana na uongozi wa juu, hatukupata majibu ya kueleweka,” amesema Irene.
Irene na wenzake wanadai hatua hiyo ya kuzuia wafanyakazi si ya kisheria na inaleta picha ya dhuluma kwa Watanzania ndani ya nchi yao.
“Muajiri wetu hajatuambia tusije kazini. Hawa wanaotufungia milango siyo waajiri wetu. Kama wana mgogoro, waumizane wao bila kutuingiza. Tunachohitaji ni Serikali itusikie. Hatuna mahali pengine pa kwenda, kazi ndiyo maisha yetu, tunawatoto na familia zetu,” amesema Irene
Wakili wa hoteli hiyo, Method Kagoma amefika eneo la tukio na kueleza kuwa hatua ya CRJE kuifungia hoteli hiyo ni kinyume cha sheria, kwani hakuna utaratibu wowote wa kisheria uliokuwa umefuatwa, licha ya madai kwamba mkataba wa upangaji umeisha.
“Jumamosi mmiliki wa jengo aliandika barua kwa mmiliki wa hoteli kumtaka aondoke ndani ya siku tatu, bila kufuata mkataba wala taratibu za kisheria. Jana wafanyakazi walizuiwa, leo wamefungiwa milango vifaa viko ndani, hakuna taarifa rasmi kutoka kwa CRJE wala agizo la Mahakama,” amesema Wakili Kagoma.
Kagoma amsema tayari wamefungua kesi katika Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara wakilalamikia kuvunjwa kwa makubaliano ya kibiashara kinyume cha utaratibu.
“Kwa sasa tumefungua kesi rasmi na tunaendelea kufuatilia hatua za mbele. Tanzania ni nchi ya sheria, na kama CRJE walikuwa na madai yao, walipaswa kwenda Mahakamani au kuomba msaada wa Serikali, si kujichukulia sheria mikononi,” amesema.
Kwa mujibu wa Kagoma, shughuli za hoteli hiyo zilianza kuyumba mwishoni mwa mwezi Aprili baada ya CRJE kukata umeme kwenye jengo, hali iliyosababisha kupungua kwa wateja.
“Wateja hawakuweza kukaa ghorofani kwa sababu ya kukosa umeme. Hii ni hasara kwa mmiliki na wafanyakazi. Wengine bado wana mikataba mipya, lakini hawajui hatma yao,” amesema.
Wafanyakazi wanatoa wito kwa Serikali kuingilia kati mgogoro huo kwa kuwa unawadhulumu watumishi wasiohusika moja kwa moja katika mvutano wa kibiashara.
“Tunaomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma. Hatujafukuzwa kazi na bosi wetu, lakini hatuwezi kufanya kazi,” alisema Ester Besta.
No comments:
Post a Comment