Katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Chapo amelakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na viuongozi wengine waandamizi wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mshauri wa Rais Mheshimiwa Angela Kairuki na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Msumbiji, Mhe. Balozi Maria Manuela dos Santos Lucas.
Mheshimiwa Rais Chapo atapokelewa rasmi Ikulu jijini Dar es Salam na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 08 Mei, 2025 na atakuwa na mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, atashuhudia uwekaji saini Mikataba na Hati za Makubaliano (MOU) katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji, atatembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika na Stesheni ya Reli ya Kisasa (SGR) jijini Dar es Salaam ili kujifunza na kuangalia fursa za ushirikiano.
Mheshimiwa Rais Chapo pia atatembelea visiwa vya Zanzibar ambapo atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt Hussein Ali Mwinyi, atatembelea miradi mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu na Soko la Samaki la Malindi.
Rais Chapo atahitimisha ziara yake nchini tarehe 09 Mei, 2025 na kuagwa rasmi na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam.








No comments:
Post a Comment