HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 7, 2025

Puma Energy Tanzania yakabidhi zawadi shindano la uchoraji kampeni ya Usalama Barabarani Mashuleni

 Kampuni ya Puma Energy Tanzania kwa kushirikiana na shirika la Amend Tanzania wamekabidhi zawadi kwa washindi wa shindano la usalama barabarani ambalo ni sehemu muhimu ya programu ya ‘Be Road Safe Africa.’ Hafla hiyo ni kielelezo cha mafanikio ya kampeni ya elimu ya usalama barabarani iliyobuniwa kuhamasisha matumizi bora ya barabara na usalama barabarani miongoni mwa vijana na wanafunzi wa shule za msingi na kuwawezesha kuwa mabalozi wa usalama barabarani ndani ya jamii zao.

Tukio lilifanyika katika Shule ya Msingi Ufukoni iliyopo Kigamboni, liliwakutanisha wanafunzi, walimu, wazazi, viongozi wa serikali na washirika wa maendeleo wa eneo hilo ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kutekeleza kampeni hii ili kuleta mabadiliko.

Akimuwakilisha Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) William Mkonda, Afisa mnadhimu wa Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Butusyo Mwambelo, ameipongeza kampuni ya Puma Energy Tanzania na Amend Tanzania kwa kuwawezesha zaidi vijana nchini kupata maarifa ya usalama barabarani yanayowawezesha kuokoa maisha.

"Mpango huu ni uwekezaji muhimu kwa mustakabali wa watoto wetu. Kwa kutoa elimu ya usalama barabarani kwa shule zilizoko kwenye barabara hatarishi, Puma Energy Tanzania na washirika wake wanahamasisha na kuokoa maisha. Ushirikiano wao na askari wa usalama barabarani ni mfano mzuri wa namna ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi unavyoweza kuleta mabadiliko yenye kuleta tija, na serikali iko tayari kuunga mkono juhudi hizi zenye kuleta matokeo chanya," alisema SACP. Mwambelo.

Awamu ya kwanza ya kampeni ya ‘Be Road Safe Africa’, ilitekelezwa mwaka 2023 and 2024, ambapo iliwafikia watoto zaidi ya 38,000 katika shule 20 za nchini Tanzania, Botswana, Zambia, na Zimbabwe. Awamu ya pili itatekelezwa katika nchi za Tanzania, Botswana, Zambia, Zimbabwe, na Afrika ya Kusini. Kwa nchini Tanzania awamu hii imezinufaisha shule tano ambazo ni: Kisukuru (Tabata), Kunguru (Goba), Mjimpya (Kurasini), Ufukoni (Kigamboni), na Salasala (Salasala).

Kampeni ya mwaka huu imewafikia zaidi ya wanafunzi 6,960 kupitia njia rahisi na shirikishi za kujifunzia, ikiwemo simulizi za hadithi, michezo - inayohusiana na masuala ya usalama barabarani na ‘Mahakama ya Watoto’. ‘Mahakama Kifani ya Watoto’ ilihusisha wanafunzi 20 wa Shule ya Msingi Ufukoni, ambapo ‘Klabu ya Be Road Safety’ ilitambulishwa. 

Wakati wa mahakama hii, wanafunzi hujifanya kama ‘majaji wa usalama barabarani’ ili kuwasaidia madereva kuelewa umuhimu wa kuzingatia usalama. Cha kuvutia zaidi, zaidi ya wanafunzi 290 wa chekechea pia walikuwa miongoni mwa wanufaika wa elimu ya usalama barabarani kupitia mpango huo.

Mashindano ya kuchora ni moja ya vipengele vinavyowavutia zaidi wanafunzi wengi katika programu hii. Wanafunzi walihimizwa kuonyesha masuala ya usalama barabarani kupitia sanaa zao. Kabla ya shindano kuanza, wanafunzi walipatiwa mafunzo kupitia warsha za mafunzo ya ubunifu katika kila shule kutoka kwa msanii maalum, akiwatia moyo na kuwawezesha watoto kuonyesha uelewa wao kuhusu usalama barabarani.

Jackson Joseph Masamakai, mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Ufukoni, Kigamboni, aliibuka kuwa mshindi wa kwanza ambapo alikabidhiwa kitita cha pesa taslimu shilingi laki tano, cheti na madaftari. Puma Energy Tanzania ilikabidhi vocha kwa ajili ya manunuzi ya vifaa vya shule ya kiasi cha shilingi milioni 5 kwa shule ya msingi Ufukoni ambayo mwanafunzi wake alishika namba moja pamoja na kikombe. 

Mshindi wa pili na wa tatu nao walizawadiwa pesa taslimu shilingi laki tatu na laki na nusu, cheti, na madaftari kwa kila mmoja pamoja. Pia, wanafunzi walioshiriki shindano hilo walipewa madaftari yenye jumbe za usalama za usalama barabrani ili kuendelea kujikumbusha pindi wakiendelea na masomo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji, Mhandisi Lameck Hiliyai amepongeza dhamira ya dhati ya wadau wote wanaohusika hususani Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Polisi wa Usalama Barabarani Tanzania.

"Tunajivunia kuona uongezekaji wa manufaa yanayotokana na programu hii na jinsi wanafunzi wanavyokuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao. Maendeleo haya yanadhihirisha ari ya washirika wetu, hasa Wizara ya Mambo ya Ndani, Elimu, na Polisi wa Usalama Barabarani Tanzania. 

Hii inadhihirisha dhamira ya Puma Energy Tanzania ya kujenga mustakabali salama kupitia sera yetu ya Afya, Usalama, na Mazingira salama (HSSE). Tunapokaribia maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani duniani, kampeni hii inaonyesha azma yetu ya kulinda maisha katika jamii tunazozihudumia,” alisema Mhandisi Hiliyai.

Katika vifo 31 kwa kila watu 100,000, WHO inaripoti kwamba vifo vinavyotokana na ajali za barabarani nchini Tanzania ni karibu mara 1.7 ya kiwango cha kimataifa na juu zaidi ya wastani wa Afrika. Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kuwa mwaka 2024 pekee, nchi ilirekodi ajali 1,735 za barabarani ambapo ajali 1,198 kati ya hizo zilisababisha vifo vya Watu 1,715. Makosa ya kibinadamu, ikiwemo kupuuzia alama za barabarani, kuendesha gari kwa uzembe, na mwendokasi, vilichangia 97% ya matukio haya.

Programu ya ‘Be Road Safe Africa’ ni sehemu ya dhamira ya Puma Energy Tanzania ya kusaidia usalama na ustawi wa jamii, hasa jamii zilizo katika mazingira magumu na maeneo hatarishi. Kupitia mafunzo ya mbinu mbalimbali, mashindano, na uboreshaji wa miundombinu, programu hii inasaidia kuzifanya barabara zetu kuwa salama kwa watoto wa shule nchini.

Afisa mnadhimu wa Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Butusyo Mwambelo, akimkabidhi mwanafunzi wa Shule ya Msingi Ufukoni, Jackson Masamaki, cheti na fedha Sh. 500,000 baada kuibuka mshindi katika mashindano ya kuchora picha zenye ujumbe wa usalama barabarani, zilizotolewa na Puma Energy Tanzania kupitia Kampeni ya Usalama Barabarani mashuleni, katika shule hiyo, Kigamboni, Dar es Salaam. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji wa kampuni hiyo, Mhandisi Lameck Hiliyai.




Afisa mnadhimu wa Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Butusyo Mwambelo, akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ufukoni, Edger Muyonga, mfano wa hundi ya Sh. milioni tano, baada shule hiyo kuibuka mshindi katika mashindano ya kuchora picha zenye ujumbe wa usalama barabarani, zilizotolewa na Puma Energy Tanzania kupitia Kampeni ya Usalama Barabarani mashuleni, katika shule hiyo, Kigamboni, Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji wa kampuni hiyo, Mhandisi Lameck Hiliyai.




Afisa mnadhimu wa Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Butusyo Mwambelo, akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ufukoni, Edger Muyonga, kombe baada shule hiyo kuibuka mshindi katika mashindano ya kuchora picha zenye ujumbe wa usalama barabarani, zilizotolewa na Puma Energy Tanzania kupitia Kampeni ya Usalama Barabarani mashuleni, katika shule hiyo, Kigamboni, Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji wa kampuni hiyo, Mhandisi Lameck Hiliyai.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad