Farida Mangube , Morogoro
Mabalozi wa nchi tano za Nordic ambazo ni Denmark, Finland, Iceland, Norway na Sweden wameupongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa mafanikio makubwa ya kuendeleza miradi ya upandaji miti na uhifadhi wa mazingira, miradi ambayo iliasisiwa kwa msaada wa mataifa hayo zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Pongezi hizo zilitolewa leo Mei 27, wakati wa ziara ya mabalozi hao mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Nordic Week hapa nchini, ambapo walitembelea kituo cha uzalishaji wa mbegu za miti kinachosimamiwa na TFS, kujionea shughuli mbalimbali za uhifadhi wa misitu na uzalishaji wa miche.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias, amesema nchi zao zinafarijika kuona mchango wao wa miaka mingi ukizaa matunda katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira nchini Tanzania. “Tumevutiwa na jitihada mnazozifanya kupitia TFS. Miradi ya upandaji miti si tu kwamba inasaidia kuhifadhi mazingira, bali pia inachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa jamii zinazozunguka misitu,” alisema Balozi Charlotta.
Kwa upande wake,Kamishna msaidizi wa uhifadhi na meneja Baiolojiaya mbegu za miti TFS Fandey Mashimba amesema taasisi hiyo itaendelea kuimarisha usimamizi wa misitu ya asili na ile inayopandwa, huku akiweka msisitizo kwenye uzalishaji wa miche bora na elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi.
“Nchi za Nordic zimekuwa washirika wa muda mrefu katika sekta ya misitu. Mafanikio tunayoyaona leo ni matokeo ya ushirikiano huo wa dhati,” amesema Naye Mkuu wa Kitengo cha Uzalishaji Mbegu wa TFS, Mohamed Msalu, ameshukuru ujio wa mabalozi hao, akisema ni ishara ya kuthamini kazi kubwa inayofanyika katika kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za miti kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
“Tunashukuru kwa ujio huu wa mabalozi wa Nordic. Umetupa hamasa zaidi ya kuendeleza juhudi zetu za kuhakikisha kuwa nchi inapata mbegu bora, zinazoweza kustahimili hali tofauti za tabianchi na kuongeza misitu,” alisema Msalu. Nordic Week ni wiki maalum ya maadhimisho yanayolenga kuonesha utamaduni, ubunifu, biashara, teknolojia na ushirikiano kutoka nchi za Nordic, huku lengo kuu likiwa ni kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii na nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania. Kwa mujibu wa mabalozi hao, mataifa yao yataendelea kushirikiana na Tanzania kupitia miradi ya mazingira, elimu, nishati mbadala na masuala ya haki za binadamu kwa ajili ya maendeleo endelevu.
No comments:
Post a Comment