Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari amezindua rasmi zoezi la ung’oaji na uchomaji wa masalia ya pamba na kuwataka wakulima wa zao hilo katika wilaya hiyo kutekeleza zoezi hilo kwa ukamilifu kwani hatosita kuwachukulia hatua za kisheria wale watakaokaidi kuchoma.
Pia amewataka maofisa ugani, watendaji wa kata na vijiji kusimamia zoezi hilo la uchomaji wa masalia ya pamba pamoja na kuhakikisha mbegu pamoja na viuatilifu vinavyotolewa na serikali vinawafikia wakulima ambao ndio walengwa wakuu.
Nassari ametoa maagizo hayo leo tarehe 22 Novemba 2024 mjini Magu wakati akizundua zoezi hilo la uchomaji masalia ya pamba ambalo limeratibiwa na Balozi wa pamba nchini, Agrey Mwanri.
Zoezi hilo lilifanyika sambamba na semina elekezi kwa maofisa ugani, watendaji wa kata, vijiji na maofisa ushirika kwa lengo la kuhakikisha elimu hiyo ya uchomaji wa masalia inawafikia wakulima kikamilifu.
Nassari amesema hatosita kutumia sheria ya pamba iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2011 kufuatilia zoezi hilo na kwa wakulima ambao watashindwa kuchoma masalia hayo watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
“Kuhusu zoezi hili, sirudi nyuma kwa sababu ni suala la kisheria lakini ni jambo ambalo linakwenda kumnufaisha mwananchi mwenyewe na lengo kubwa ni kumpeleka kwenye mafanikio,” alisema.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Mohamed Ramadhani amewataka maofisa ugani, watendaji wa kata na vijiji kuwajengea uelewa wa kutosha wakulima kuhusu ulimaji sahihi wa zao la pamba badala ya kurudia kila mara namna ya kupanda zao hilo na namna ya kutumia viuatilifu.
“Hii ni changamoto ambayo inawasumbua sana wakulima wetu kwa sababu tangu miaka ya 1970 wakulima wetu wamekuwa wakifundishwa namna ya kupanda kwa mpangilio na kupulizia viuatilifu… hatupigi hatua kuelekea kwenye mambo mengine, kila mra ni kurudia kilekile, hivyo nawaomba watendaji mhakikisha elimu hii inawafikia kikamilifu badala ya kurudia tena mwakani kuwafundisha,” amesema.
Naye Balozi wa pamba Tanzania, Agrey Mwanri amesema hii ni mara ya pili anatoa elimu kwa wakulima wa Magu kuhusu umuhimu wa kung’oa masalia ya pamba na amebaini kuwa ni wakulima wachache waliochoma masalia hayo kwa mwaka huu.
“Ninachokuomba mhe. Mkuu wa wilaya ni hili suala la uchomaji wa masalia yap amba kwa sababu ni jambo linalotakiwa kusimamiwa kikamilifu. Tangu tarehe 15 Septemba wakulima walitakiwa kuchoma masalia hayo, serikali nayo iliongeza muda hadi Oktoba 15 lakini hadi sasa wakulima hawa hawajachoma.
“Na usipochoma masalia hayo ndipo unaposababisha wadudu kuvamia shamba lako katika msimu unaofuata na kupungua mavuno yako ndio maana tunawasisitiza kuchoma. Pia wasichanganye zao hili la pamba na mazao mengine. Kwa mfano mahindi yanatumia siku 90 kukomaa, lakini pamba siku 150 kwa hiyo ni uhalisia kwamba pamba itanyonywa na mahindi hivyo kukotostawi kwa ubora unaotakiwa,” alisema.
Thursday, November 21, 2024
Home
Unlabelled
Magu yazindua kampeni ya uchomaji masalia ya pamba
Magu yazindua kampeni ya uchomaji masalia ya pamba
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment