WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) ameanza ziara ya kikazi katika Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora ambapo ameanzia kwa kukutana na Viongozi wa Bodi ya Pamba, Wafanyabiashara, Wawekezaji na Wakulima wa Pamba tarehe 11 Septemba 2024.
Amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa na ana nia ya dhati ya kuinua Sekta ya Kilimo, hivyo ni wakati wa Halmashauri nchini kuwa sehemu ya kutekeleza maono hayo kwa kuinua uchumi ili kusaidia kuondoa umaskini.
Serikali za Wilaya na Mikoa mna wajibu wa kusimamia mabadiliko haya, tunaleta kwenu Maafisa Ugani ili waje kuwa chachu ya mabadiliko katika Sekta ya Kilimo, watumieni ipasavyo,” amesema Mhe. Waziri Bashe.
Aidha, Mhe. Waziri Bashe amesema Maafisa Ugani hao wahakikishe kila Kata kunakuwa na zao la uzalishaji lenye matokeo ya baadaye katika kijiji.
“Lazima tupimane kwa matokeo ya kiuchumi, katika suala la uzalishaji tusiruhusu siasa. Zao la Pamba ni muhimu sana katika uchumi kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa,” amesisitiza Mhe. Waziri Bashe.
Akitoa taarifa ya utendaji, Bw. Marco Charles Mtunga, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba amesema kuwa ziara hiyo ni muhimu kwa Wilaya ya Igunga kwa kuwa inazalisha zao la Pamba kwa kiasi cha takribani tani 22,000 hadi 26,000.
Ameongeza kuwa hatua ya Wilaya hiyo kuwezeshwa zana bora za kilimo, mafunzo na kupatiwa Maafisa Ugani itakuwa na uwezo wa kuzalisha hadi tani 100,000 ambapo kwa kila mkulima ni wastani wa uzalishaji ni kilo 300 (ambayo ni tani 0.3).
Kwa sasa, zao la Pamba nchini linazalishwa kwa tani 284,000 ambapo malengo ya nchi no kuwa na uzalishaji wa tani 500,000.
No comments:
Post a Comment