Meneja wa Mkoa wa Dodoma wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),Mkadiriaji Majenzi, Qs. Emanuel Wambura,akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda TBA kwenye Maonesho ya Kilimo Kitaifa ya Nane Nane, yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni,jijini Dodoma
*Yajenga Vihenge vya kuhifadhi mazao katika Mikoa Mitatu
Na Chalila Kibuda,Michuzi TV Dodoma
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) imesema kuwa imejipanga katika kuhakikisha Wakulima, Wafugaji pamoja na Wavuvi wanakwenda kuondokana na changamoto ya kuhifadhi mazao yao.
Hayo ameyasema Meneja wa TBA Mkoa wa Dodoma Mkadiriaji Majenzi, Qs. Emmanuel Wambura wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la TBA katika Maonesho ya Kitaifa ya Nane Nane, yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni,jijini Dodoma.
Wambura amesema TBA umetumia Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ujenzi katika Sekta ya Kilimo na Ufugaji,pamoja na Uvuvi.
Amesema kuwa TBA inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kuelimisha miradi ya ujenzi inayotekelezwa na wakala huo, hususan katika sekta hizo.
Hata hivyo Wambura ameongeza kuwa TBA inaendelea kushirikiana na wakulima kwa kuwashauri juu ya mbinu bora za ujenzi wa nyumba za makazi na kuboresha miundombinu ya biashara ya mazao yao.
Amesema kuwa katika jitihada hizo wamejenga vihenge vya kuhifadhi mazao yao katika Mikoa Mitatu ya Manyara ,Rukwa pamoja na Katavi huku Mikoa mitano ikiendelea na ujenzi wa Vihenge hivyo.
Wambura amesema uboreshaji wa miundombinu katika hizo imechangia kuleta ufanisi katika biashara ya mazao ya kilimo pamoja na kusimamia mradi mkubwa wa ujenzi wa vihenge na maghala ya kuhifadhia chakula.
“Mradi huu ni wa muhimu sana kwa wakulima kwani unawasaidia kuhifadhi mazao kama mahindi, ambayo yanapata thamani zaidi kabla ya kupelekwa sokoni,”amesema Wambura
Aidha amesema miradi ya kilimo, TBA pia imetekeleza miradi katika sekta ya mifugo kwa kubuni kujenga soko la mnada wa mifugo katika Mkoa wa Geita.
No comments:
Post a Comment