Mwamvua Mwinyi,Pwani
KAYA za wanufaika 18,403 wa mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) Mkoani Pwani, wamehitimu katika mpango huo kufikia Juni 2024.
Akitoa taarifa kikao cha mwaka cha utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) ,Mratibu wa TASAF Mkoani Pwani, Roselyn Kimaro alisema ,taratibu zikikamilika walengwa hao watakuwa wamejiondoa kwenye mpango baada ya kuandaliwa vizuri na sasa wamefanikiwa.
Alisema, mpango huo unatekelezwa katika Halmashauri 9 zenye ,jumla ya Kata 133 na vijiji 417 na mitaa 73, hadi Juni, 2024 kaya za wanufaika 18,403 zimehitimu ambapo kaya 17,761 zinazoendelea kunufaika zikiwa ni kaya katika vijiji vipya vya 30.
Hata hivyo, alieleza, mkoa unaendelea na utekelezaji wa shughuli za Mpango kwa kipindi cha pili kilichoanza mwaka 2020 kwa lengo la kuendelea kupunguza kiwango cha umaskini kwa kuhakikisha wananchi wanapata mahitaji muhimu, kuboresha maisha ya kaya na mtu mmoja mmoja kwa kutoa fedha taslim kwa kila kaya.
"Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha kiasi cha sh.bilioni 40.372.2"
Roselyn alifafanua, fedha hizo zimetumika kukuza uchumi wa kaya kwa ruzuku za elimu na afya, upatikanaji wa chakula na uboreshaji wa miundombinu ya elimu, afya, soko ,ujuzi na stadi za maisha kwa walengwa walioshiriki miradi ya ajira za muda (PWP).
Vilevile Roselyn alitaja mafanikio, ikiwemo sh. bilioni 28.7 zimetolewa kama ruzuku fedha taslimu kwa kaya kwa lengo la kuimarisha uchumi wa kaya, kupata chakula milo mitatu na kuwezesha watoto shule na kliniki.
Pia jumla ya miradi ya miundombinu ya afya, maji na elimu 13 yenye thamani ya sh.bilioni. 2.2 imetekelezwa katika ngazi wilaya ambapo miradi sita tayari inatoa huduma.
Aidha mratibu huyo anasema, kuna miradi ya ajira za muda (PWP) 647 yenye thamani ya sh.bilioni 4.5 imetekelezwa na wanufaika ambao wameweza kupata ujira, ujuzi na huduma.
Alisema kuwa, hadi Juni 2024 wanufaika 15,740 sawa na asilimia 50 ya wanufaika 31,697 wameweza kujiunga na mfumo wa upokeaji wa ruzuku kwa njia ya mtandao(Simu na Banki) baada ya Mkoa kupitia Halmashauri kutoa elimu ya utumiaji wa teknolojia ya simu.
Pamoja na hayo ,TASAF kipindi cha pili wanafunzi 96 wameweza kujiunga na vyuo vikuu wakiwemo wasichana 50 na wavulana 46 sambamba na wanafunzi 194 wamejiunga na vyuo vya kati wanaume 104 na wanawake 90.
Roselyn alitaja mafanikio mengine kuwa ni, upatikanaji wa mitaji kupitia vikundi 1,309 vya kuweka akiba na kukopa vya wanufaika wa mpango vyenye idadi ya watu 17,195 ambapo wanawake 15,494 na wanaume 1,701.
"Mafanikio makubwa yamepatikana hadi Juni 2024 vikundi vimekusanya mtaji wa Tsh.500,808,213 Vikundi vimesajiliwa na Serikali kupitia TASAF pamoja na mfumo wa BOT"alisema Roselyn.
Mnufaika Ramadhani Selemani aliishukuru serikali kupitia mpango huo na kusema unainua maisha ya kaya maskini.
Ramadhani alieleza, kipindi cha nyuma alikuwa akiishi kwenye nyumba ya udongo lakini sasa amejenga nyumba kwa kutumia tofali na anaweza kujikimu kimaisha kupitia shughuli ndogondogo.
"Nipo tayari kujiondoa katika mpango huu, nashukuru serikali kwa kutubeba na kwa hakika imekuwa mkombozi wa kaya maskini "alieleza Ramadhani.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani,alhaj Abubakar Kunenge aliipongeza TASAF mkoa chini ya mratibu Roselyn kwa mafanikio waliyoyapata.
Alisema ,wameonyesha usimamizi mzuri wa fedha za utekelezaji mpango na wanafanya kazi kubwa.
No comments:
Post a Comment