HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 20, 2024

DC CHACHA APIGA MARUFUKU UPENDELEO KATIKA UGAWAJI WA PEMBEJEO ZA RUZUKU

 Na Mwandishi Wetu, Tunduru

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Simon Chacha,amewataka Viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika(Amcos)Wilayani humo,kuacha upendeleo kwenye ugawaji wa pembejeo za ruzuku zinazotolewa bure na Serikali ili kila mkulima aweze kunufaika na pembejeo hizo zinazotumika kwa ajili ya kupulizia mikorosho.

Alisema,hatua hiyo itajenga imani,kuleta mshikamano na kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima kati yao na wanachama wao wanaowaongoza.

Chacha alisema hayo jana,alipokuwa akizungumza na baadhi ya wakulima wanaohudumiwa na Chama cha msingi cha Ushirika cha Mtetesi Amcos, baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wakulima wa vijiji vinne vya Mtonya,Mindu,Liwangula na kitingoji cha Mjimwema wakilalamika kukosa mgao wa dawa aina ya Sulphar, hivyo kushindwa kuendelea na maandalizi ya kilimo cha zao la korosho katika msimu 2024/2025.

Chacha alisema,iwapo viongozi ambao ni wasimamizi wa Amcos hizo watafanya shughuli kwa misingi ya upendeleo na kutanguliza maslahi binafsi ,basi juhudi za kufikia malengo kupitia sekta ya ushirika zitakwama.

Alisema,ili malengo ya chama yaweze kufikiwa ni muhimu kwa viongozi wa Ushirika kufanya kazi kwa kufuata sheria,usawa,kutenda haki,uwazi na uwajibikaji na kukumbuka malengo ya kuanzishwa kwa Ushirika ili wanachama wapate mkombozi katika harakati za kupambana na umaskini.

“nidhamu,uadilifu na usimamizi wa majukumu sehemu ya kazi ni kitu muhimu sana,hivyo ni lazima kila mmoja awajibike kutokana na sehemu na nafasi aliyopo ili kujenga utendaji bora na wenye maslahi mapana kwa wanachama”alisema Dc Chacha.

Alisema,hata wanachama ni chanzo cha kukosa pembejeo kwani walitoa taarifa za uongo wakati wa zoezi la kuhakiki mashamba yao kabla ya kuanza kwa usambazaji wa pembejeo kwenye vyama vya msingi vya ushirika.

“Tatizo lingine ni nyinyi wakulima mna tabia ya kusema uongo mnapotakiwa kutoa taarifa sahihi za uhakiki wa mashamba yenu,ninazo taarifa baadhi yenu mnawaacha wataalam wetu waende mashambani pekee yao”alisema Chacha.

Hata hivyo,amewataka wakulima wilayani humo,kuwa wakweli na kutoa taarifa sahihi linapokuja suala la uhakiki wa mashamba yao,kwani uongo wao unachangia sana kukosa haki zao za msingi.

Amewaomba kutoa michango ya mali au mawazo ya kujenga yatakayosaidia kupatikana maendeleo ambayo yatawezesha kufikiwa malengo kwa kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake meneja wa Chama kikuu cha Ushirika(TAMCU ) wilayani humo Marcelino Mrope alisema,katika mapokeo ya Sulphar katika msimu wa kilimo 2024/2025 maghala matatu yamehusika ambayo ni ghala la Chama kikuu cha Ushirika,ghala la chama cha msingi Namiungo na Namitili Amcos.

Mrope,amekiri wakulima wa Chama cha Namitili na Namiungo Amcos wamepata mgao wa Sulphar mara mbili ikilinganishwa na wakulima wa vijiji vingine kutokana na maghala yake kuwa na sifa.

Meneja wa chama cha msingi Mtetesi Amcos Fadhil Lada alisema,wamepokea jumla ya mifuko ya Sulphar 5,040 ambapo mifuko 4,640 imegawiwa kwa wakulima na 400 imebaki ghalani kwenye ghala kwenye ghala la chama hicho.

Alisema,chama hicho kinahudumia wakulima zaidi ya 1,750 na waliopata dawa ni 1,200 kwani siyo wakulima wote walima korosho huku baadhi ya wachache wamepata mgao pili.

Alisema,wakulima 20 hawajapata kabisa pembejeo hivyo hizo zilizobazi zitagawiwa kwa wakulima wasiopata na changamoto kubwa imesababishwa na wakulima kutopatikana kwenye zoezi la uhakiki wa mashamba yao.
 Mkulima wa zao la korosho wa kijiji cha Mtonya kata ya Mindu wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Hulberth Wale,akizungumza kwenye mkutano kati ya wakulima wa zao ulioitishwa na Mkuu wa wilaya ya Tunduru Simon Chacha ili kupata suluhu ya upatikanaji wa pembejeo kwa ajili ya zao la korosho.
Baadhi ya wakulima wa zao la korosho wanaohudumiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika Mtetesi Amcos kilichopo kata ya Mindu wilayani Tunduru,wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Tunduru Simon Chacha(hayupo pichani) wakati wa Mkutano wa Mkuu wa wilaya na wakulima hao uliolenga kutafuta suluhu ya changamoto ya upatikanaji wa dawa za kupulizia mikorosho zinazotolewa bure na Serikali.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Simon Chacha,akizungumza jana na wakulima wa zao la korosho wanaohudumiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika Mtetesi Amcos ambao wamelalamika kukosa mgao wa pili wa dawa za kupulizia korosho Sulphar zilizotolewa bure na Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad