HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 7, 2024

KWA MARA YA KWANZA NCHINI MUHIMBILI MLOGANZILA YATUMIA NJIA YA MATUNDU MADOGO KUONDOA MAWE KWENYE NJIA YA MKOJO

 


Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Mkojo (TAUS) kwa mara ya kwanza nchini wamefanya upasuaji wa kuondoa mawe kwenye njia ya mkojo kwa kutumia matundu madogo kwa wagonjwa waliokuwa na changamoto za mawe kwenye njia mkojo.Akielezea huduma hiyo, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa mfumo wa Mkojo, MNH Mloganzila Dkt. Hamis Isaka amesema lengo la huduma hiyo ni kuendelea kupanua wigo wa matibabu kwa wagonjwa wenye changamoto za mawe kwenye njia ya mkojo na huduma hizo zitakuwa endelevu.


“Baada ya kufanya kwa mafanikio huduma ya kuvunja mawe kwenye figo na mfumo wa mkojo kwa kutumia mawimbi mtetemo, hospitali imeamua kuanzisha huduma ya kutoa mawe kwenye njia ya mkojo kwa kutumia matundu madogo sambamba na matibabu ya kuzibua njia ya mkojo kwa kutumia mashine maalum ya leza” amebainisha Dkt. Isaka


Dkt. Ameongeza kuwa kuwepo kwa huduma hizi kutamuwezesha mgonjwa afanyae uchaguzi wa huduma anayohitaji kufanyiwa kwa kuzingatia ukubwa wa tatizo alilonalo kwa kuzingatia ushauri kutoka kwa wataalam wa huduma hizo.


Dkt. Isaka amefafanua kuwa umuhimu wa huduma ya matundu madogo ni pamoja na mgonjwa kutokuwa na kovu kubwa, kukaa hospitali kwa muda mfupi takribani siku mbili badala ya wiki moja ambayo angetumia mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kawaida na pia kurejea katika majukumu yake katika muda mfupi zaidi.


Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeendelea kuanzisha huduma za ubingwa bobezi ambazo hazipatikani nchini na kuwapunguzia Watanzania gharama na usumbufu wa kutafuta matibabu hayo nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad