HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 11, 2024

DKT. NCHEMBA: UJENZI WA KITUO CHA FORODHA HUZINGATIA UCHUMI NA USALAMA

 Na. Peter Haule, WF, Dodoma


Waziri wa Fedha m, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amemshauri Mbunge wa Ngara, Mhe. Ndaisaba George Ruhoro kushirikiana na Mamlaka husika ili kuangalia uwezekano wa ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Mugoma, mkoani Kagera baada ya kujiridhisha pasipo shaka iwapo eneo hilo linafaa kwa ujenzi wa Kituo hicho.

Mhe. Dkt. Nchemba alisema hayo bungeni, jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ngara, Mhe. Ndaisaba George Ruhoro, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Mugoma.

Alisema kuwa endapo Mamlaka husika zitajiridhisha pasipo shaka kuhusu eneo hilo kutokuwa na madhara kwa nchi kiuchumi, kijamii na kiusalama, Serikali itashauriwa kuyafanyia kazi maombi hayo.

“Kabla ya eneo au kituo kuteuliwa kuwa eneo la Forodha na kuweza kufunguliwa kama kituo cha forodha mahali popote nchini kuna taratibu za kisheria ambazo inabidi zifuatwe”, alisema Dkt. Nchemba.

Alieleza utaratibu huo kuwa ni pamoja na kutangazwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya Mwaka 2004, Kifungu Namba 11.

Dkt. Nchemba alisema kuwa baada ya Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa kupokea maombi ya kuteua eneo husika kuwa eneo la forodha kutoka kwa Waziri mwenye dhamana, huwasilisha pendekezo la kuteua kituo husika kwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Ngara, Mhe. Ndaisaba George Ruhoro, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Mugoma.

.

 (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- Wizara ya Fedha)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad