HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 6, 2024

SERIKALI yabuni miradi ya kimazingira kusaidia jamii kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi

 

SERIKALI imesema imebuni miradi mbalimbali ya kimazingira inayosaidia jamii kuweza kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali nchini.


Pamoja na hatua hizo pia, imeendelea kuihimiza jamii kutumia nishati mbadala na majiko banifu ili kupungunguza kasi ya ukataji wa misitu ambayo husababisha uharibifu wa mazingira.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi wakati akijibu maswali bungeni kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo bungeni jijini Dodoma leo tarehe 06, 2024.


Akijibu swali la Mbunge wa Mwera Mhe. Zahor Mohammed Haji aliyetaka kujua mpango wa Serikali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika kuwakinga wananchi na madhara yanayoweza kutokea, Mhe. Katambi amesema Serikali inatekeleza miradi ya upandaji miti, usambazaji wa maji safi kwa matumizi ya majumbani na mifugo na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.


Ametaja ujenzi wa kuta katika maeneo ya fukwe za bahari yanayokabiliwa na mmomonyoko wa ardhi, ujenzi matuta na mabwawa kudhibiti mafuriko, kuwezesha jamii kubuni miradi mbadala ya kuongeza kipato na iliyo rafiki kwa mazingira pamoja na urejeshaji wa maeneo ya ardhi yaliyoharibika kuwa ni jitihada zingine za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.


Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Katambi amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021), Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) na Mchango wa Taifa katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021) ambayo ina mchango katika kukabiliana na changamoto hiyo.


Ameongeza kuwa Serikali inashirikiana kikamilifu na jumuiya ya kimataifa katika kubuni mikakati na hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika ngazi zote ikiwemo kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris.


Aidha, Naibu Waziri Katambi amesema Serikali inaendelea kuelimisha wananchi kuhusu madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi ili waweze kuchukua tahadhari na kujilinda na maafa yanayosababishwa na changamoto hizo, ambapo uelimishaji hufanyika kabla ya maafa kutokea.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad