HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 17, 2024

SERIKALI KUJIKITA KWENYE KINGA YA MARADHI ZAIDI YA TIBA

 

Waziri wa Afya nchini, Ummy Mwalimu akizungumza na watafiti kutoka sehemu mbali mbali nchini wakati wa kufunga mkutano wa 32 wa wanasayansi ulioanza Mei 14, hadi leo Mei 16 2024. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Profesa Said Aboud akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa 32 wa wanasayansi ulioanza Mei 14, hadi leo Mei 16 2024. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam ambapo wanasayansi kutoka sehemu mbali mbali nchini wamekutana na kujadili magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyoambukiza na ubunifu pia.
Mjumbe wa Bodi ya wadhamini NIMR Dkt. Ntuli Kapologwe


SERIKALI imesema kuwa kuwa itaimarisha mifumo ya utoaji huduma ya kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ili kuweza kumuepusha mtanzania kupata magonjwa au kugundua magonjwa katika hatua ya awali.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema hayo leo Mei 16, 2024 wakati wa akifunga Mkutano wa 32 wa wa Wanasayansi uliofanyika kwa siku tatu kuanzia Mei 14 jijini Dar es Salaam uliokuwa umeandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR)

Waziri Ummy amesema kuwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya sita kutafuta kinga ya maradhi ili kuokoa fedha zinazotumika kwenye kununua dawa na vifaa tiba.

"Nimekuwa nikiwaambia wenzangu mimi ni waziri wa afya na afya ni kuzuia kwanza watu wasiugue halafu ndio yanakuja masuala ya tiba, lakini sasa tunakuwa ni watu wa kulilia dawa na kama tutaenda na mwenendo huu dawa basi hazitatosha... Hivyo tunaweza kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa ikiwa tutawekeza pia kwenye huduma za kinga na tiba" amesema waziri Mwalimu.

Waziri Ummy Pia amewataka watafiti wote nchini kizingatia sheria na kanuni za kufanya tafiti za afya ikiwemo kuhakikisha zinapata kibali cha NIMR ili kuendelea kufanya tafiti zenye tija nchini huku pia akiwaasa NIMR kutokuweka vikwazo mkubwa kwa tafiti muhimu.

"Mnafanya tafiti nyingi na nzuri lakini kama hatuzijui itakuwa haina tija, mmefanya tafiti nyingi na nzuri lakini kama wanasiasa hatuzijui zitabaki kuwa ni tafiti za kwenye makaratasi hivyo nawaomba muimarishe utaratibu wa kujitangaza na kutangaza tafiti zenu. Tumieni waandishi wa habari hawa muwaeleze mlichofanya mlichogundua na matarajio yake". Amesema Ummy

Wakati huo huo Waziri Ummy amewapa changamoto watafiti juu ya kufanya utafiti wa tunda la Stafeli juu ya matibabu ya saratani ili kusaidia matibabu.

Sisi tunasikia maneno kwamba tunda la stafeli linatibu saratani sasa nyie ndio watafiti mtuambie kinachotibu ni tunda, majani au mizizi, watanzania wangependa kusikia, watu wanakula mavitu mengi hivyo watafiti fanyieni utafiti ili tupate kujua ukweli. Fanyeni tafiti zinazojibu changamoto za watanzania na maswali yao.

Pia waziri Ummy amewataka watafiti kufanyia tafiti dawa za auntbiotic hususani UTI, kwani imekuwa namba nne katika wagonjwa wa nje hivyo waje na tafiti zinazoonyesha majibu sahihi ya vipimo vya UTI

Waziri Ummy ameongeza kusema kuwa atahakikisha kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya utafiti zitatolewa mapema ili kuharakisha zoezi hilo.

Kwa upande wake, Profesa Said Abuod Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) amesema katika mkutano huo wamejadili mada 241 zilizowasilishwa na watafiti.

Amesema kuwa Mkutano huo ulikuwa na makongamano madogo matano yaliyojadili kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya, maradhi yanayoambukiza, Malaria, Ukimwi, na kifua kikuu.

Amesema kuwa mafanikio ya mkutano huo ni ushiriki wa watunga sera na wafanya uamuzi waliohudhuria kwenye mkutano huo.

"Jukumu la NIMR ni kufanya utafiti kwa niaba ya Serikali na matokeo ya utafiti huo utakaosaidia uamuzi kwenye kutunga sera, kufanya uamuzi wa Kisayansi na kuboresha huduma za Afya .

Naye, Mjumbe wa Bodi ya wadhamini wa NIMR Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa NIMR itahakikisha inafanyia kazi tafiti zenye kutoa suluhisho la matatizo kwenye jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad