HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 28, 2024

RPC KINONDONI AAHIDI KUTOA USHIRKIANO KUKAMATWA BASI LA KILIMANJARO

  



KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, RPC Mtatiro Kitinkwi ameieleza mahakama kuwa atatoa ushirikiano kukamatwa kwa basi la Kampuni ya Mabasi ya Kilimanjaro lenye namba T 178 EAU, ambalo aliliruhusu liendelee na safari wakati lilikuwa limekamatwa na dalali wa mahakama.

RPC Kitinkwi alifika juzi katika Mahakama Kuu Kanda la Dar es Salaam, baada ya kupata wito wa mahakama ili ajieleze kwa nini alikiuka amri ya mahakama ya kukamatwa kwa gari hilo lililotakiwa liuzwe ili familia ya Leonard Kisenha ilipwe fidia, baada ya kusababisha kifo cha Immaculate Kisenha (16) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha tano.

Msajili Sundi Fimbo wa mahakama hiyo, alimtaka RPC ajieleze kwa nini alifanya hivyo, alidai kuwa alipokea simu kutoka kwa abiria akilalamika kuzuiliwa kuendelea na safari eneo la Shekilango, Dar es Salaam, kibinadamu akawaruhusu waendelee na safari kwa sababu kupeleka basi lingine kwa wakati huo ilikuwa ngumu.

"Kwa sababu magari huwa yanakaguliwa kabla ya kuanza safari, kwa hiyo nikaona kuruhusu gari lingine ambalo halijakaguliwa lingeleta shida akaruhusu liende halafu kesho yake (Mei 16,2024 ) saa saba mchana lipelekwe Kituo ch Polisi Oysterbay,"alidai RPC Kitinkwi

Baada ya kueleza hayo aliahidi kuwa atatoa ushirikiano kukamatwa kwa basi hilo na kurudishwa kwa dalali wa mahakama ambae ni Daniel Mbuga wa Legit Auction Mart.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Rowland Sawaya alipoulizwa na mahakama kama na yeye alihusika kuzuia basi hilo alidai kuwa hakuzuia na pia yeye hajui mambo ya sheria. Mkurugenzi huyo tangu shauri hilo lilipofunguliwa hakuwahi kufika mahakamani hadi alipoandikiwa hati ya kukamtwa.

Baada ya hayo, Msajili Fimbo alitoa amri kuwa utekelezaji uendelee gari zikamatwe zenye namba T 178 EAU na T 508 DDB zikishakamatwa dalali alete mrejesho kwa mahakama ili aweze kupata ruhusa ya kuyauza. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 3,2024.

Wakili wa wadai hao, Mngumi Samadani akiwa nje ya mahakama alidai kuwa mahakama hiyo ilifikia hatua hiyo, baada ya kuwasilisha hoja mahakamani mkutokana na dalali wa mahakama kuzuiliwa kukamatwa kwa gari hilo wakati tayari mahakama ilishatoa amri.

Wadaiwa katika shauri hilo namba 47,2022 ni Kampuni ya Kilimanjaro Truck Ltd, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Rowland Sawaya na Mjahidi Mohamed aliyekuwa dereva wa basi lililosababisha ajali lenye namba za usajili T 278 ALQ aina ya Scania

Awali, akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya Jaji Leila Mgonya, Msajili wa Mahakama Kuu, Joseph Luambano alisema wadaiwa wanatakiwa kulipa fidia ya Sh milioni 300 kwa kusababisha kifo, majeruhi na uharibifu wa gari hilo.

Pia, alisema watakapochelewesha malipo hayo watatakiwa kulipa riba ya asilimia saba kila siku kwa mwaka na pia wadaiwa watatakiwa kulipa gharama za kesi hiyo na kwamba haki ya rufaa ipo wazi.

Kisenha alifungua kesi hiyo ya madai namba 47, 2022 baada ya kupata ushindi katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ambayo ilimtia hatiani Mjahidi katika kesi ya trafiki kwa kukiri kuendesha gari hilo bila kuwa na bima, kusababisha kifo, majeruhi Omenis Kabora na uharibifu wa gari aina ya Toyota Land cruiser lenye namba za usajili T 323 CWB .

Kisenha ambaye ni baba wa marehemu Immaculate, Desemba 24, 2021 akiwa na watoto wake wawili na mke wake walikuwa safarini kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.

Alisema walipofika eneo la Kamala Bagamoyo saa 10:15 alfajiri basi la Kilimanjaro liliacha njia na kuwagonga hivyo kusababisha kifo cha Immaculate papo hapo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad