HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, May 25, 2024

MAMIA YA WASHIRIKI KATIKA MBIO ZA RUN FOR BINTI

Mei 25, 2024, Dar es Salaam: Washiriki zaidi ya 700 walishiriki katika mbio za Run for Binti zilizofanyika katika Viwanja vya Oysterbay, ikiwa ni msimu wa tatu wa mafanikio wa mbio hizi zinazoratibiwa na kuandaliwa na Smile for Community (S4C) kwa kushirikiana na Legal Services Facility (LSF). Lengo kuu la mbio hizi ni kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu bora, afya ya uzazi, utunzaji wa mazingira, na kuimarisha afya kupitia mazoezi.

Mbio hizi zilijumuisha aina mbalimbali za mashindano, ikiwemo mbio za kilomita 21, kilomita 10, na kilomita 5. Washiriki walionekana wakiwa na hamasa kubwa ya kushiriki, huku wakifanikisha malengo ya kuwasaidia watoto wa kike kupata hedhi salama na mazingira bora ya kujifunzia. Mgeni rasmi, Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Pindi Chana, kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mh. Dkt. Doto Biteko, aliongoza mamia ya washiriki katika mbio hizo.

Akitoa hotuba yake wakati wa mbio hizo, Mh. Dkt. Pindi Chana alisema, "Niwapongeze LSF kwa kushirikiana na Smile for Community kwa kuandaa mbio hizi ambazo zimeweza kutuleta pamoja. Kama serikali, tunatambua na kuthamini juhudi zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kusaidia maendeleo ya jamii na kutatua changamoto zinazowakabili watoto wa kike hivyo tunaunga mkono jitihada hizi. Aidha Serikali tumeanza kampeni maalumu inayowasisitiza wananchi kufanya mazoezi hii ni fulsa nzuri sana kwa wananchi kushiriki na kutimiza hili. Aidha tunatambua changamoto mbalimbali zinazowakumba jamii hususani katika hedhi salama lakini uhitaji wa miundo mbinu kwa maeneo yenye changamoto hivyo kwa kupitia ushirikiano huu, tutaweza kuboresha zaidi maisha ya watoto wa kike na jamii kwa ujumla.

Akiongea wakati wa mbio hizo, Flora Njelekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Smile for Community, alitoa shukurani kwa mgeni rasmi kwa kuridhia na kuipa uzito mbio hizi kwa kuwa pamoja nasi leo hapa. "Hii inaonesha wazi kuwa Serikali inaunga mkono juhudi zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kutatua changamoto za kijamii," alisema Njelekela. Pia alibainisha matokeo yanayotarajiwa baada ya mbio hizo. "Fedha zilizokusanywa leo zitaelekezwa moja kwa moja kwenye ujenzi na kuboresha miundombinu ya vyoo, kutoa maji safi kwa kujenga visima mashuleni, na kusambaza taulo za kike zinazoweza kutumika tena, kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi na matumizi sahihi ya nishati safi. Juhudi hizi tayari zimewanufaisha maelfu ya wanafunzi katika shule za sekondari za Mtwara, na tutaendelea kuongeza wigo kufikia shule nyingi zaidi huko Lindi na kwingineko.

Aidha Njelekela ametumia fulsa hiyo kuiomba serikali iweze kuondoa kodi kwa taulo za kike ili kuongeza upatikanaji na gharama nafuu, kwani uhitaji wa bidhaa hizi kwa watoto wa kike na wanawake ni mkubwa na wengi hawawezi kumudu gharama hizi kila mwezi."

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Bi. Lulu Ng'wanakilala, alisisitiza changamoto zinazoendelea kukabiliwa na watoto wa kike na umuhimu mkubwa wa miradi kama hii katika kupambana na vikwazo hivyo. "Katika jitihada zetu za kutoa huduma za msaada wa kisheria, tunaona moja kwa moja vikwazo wanavyokutana navyo watoto wa kike. Mbio za leo ni zaidi ya mashindano; ni harakati kuhakikisha tunatengeneza jamii inayomuinua na kumlinda mtoto wa kike na kuhakikisha kwa pamoja tunaweka rasilimali na nguvu za pamoja katika kutatua changamoto za jamii, lakini pia tunajenga afya zetu. Niwashukuru sana mamia ya wananchi waliotuunga mkono kwa kuchangia na kushiriki mbio hizi leo."

Nae mdhamini mkuu wa mbio hizi, Benki ya Stanbic, walieleza kuwa mbio hizi zinaenda sambamba na vipaumbele vyao vya kusaidia jamii kielimu, kiuchumi, na kiafya, na hivyo imevutiwa sana na matokeo ya mbio hizi kwa mwaka jana. Stanbic itaendelea kushirikiana na LSF pamoja na Smile for Community katika kuratibu na kuandaa mbio hizi kila mwaka.


Waziri wa Katiba na Sheria Balozi, Dkt Pindi Chana akiwa pamoja Mkurugenzi Mtendaji wa LSF Bi. Lulu Ng'wanakilala na Mkurugenzi Mtendaji wa Smile For Community Bi. Flora Njelekela na washiriki wengine wakishiriki katika mbio za Hisani za Run For Binti Marathon ambazo zimefanyika kwa msimu wa tatu sasa zenye lengo ya kumuinua Mtoto wa Kike Kiuchumi na Kijamii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad