HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 24, 2024

SERIKALI YAIPONGEA SUA KWA KUJA NA MBUNI ZA KULINDA UKANDA WA MAGHARIBI MWA BAHARI YA HINDI.

Na: Calvin Gwabara – Mbeya.


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera kwa niaba ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepongeza kazi nzuri ya Utafiti
iliyofanywa na SUA kwa kushirikiana na NEMC na kupelekea matokeo yake
kusambazwa kwenye nchi kumi zilizo ukanda wa magharibi mwa Bahari ya
Hindi.

Pongezi hizo zimetolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya
Mhe. Beno Malisa wakati akifunga mafunzo ya siku sita kwa Maafisa
Waandamizi wa Masula ya Maji na mazingira kutoka kwenye nchi nne
ikiwemo Madagaska,Msumbiji,Kenya na mwenyeji Tanzania ikiwa ni
sehemu ya kusambaza matokeo ya Mradi wa Utafiti wa Usimamizi
Endelevu wa Madakio ya Maji Kupitia Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko
wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji wake katika Kulinda Ukanda wa
Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Athari za Shughuli za Kibinadamu
Tanzania (EFLOWS).

“Kwa niaba ya Mkoa wa Mbeya nitumie nafasi hii kukipongeza Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo kupitia kwa Mtafiti Mkuu wa Mradi huu wa
EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili amabye ndiye mratibu wa mafunzo haya
kwa kazi nzuri waliyoifanya hadi sasa ambapo tunaona matokeo yake
yamewezesha nyinyi nyote kukutana nchini Tanzania ili kuona na kujifunza
matokeo mazuri kwa lengo la kwenda kuyatumia kwenye nchi zenu ili
kulinda mtiririko salama wa maji kuelekea baharini” alifafanua Mhe.Malisa
.
Amesema anaamini kuwa elimu waliyoipata kupitia Wataalamu wabobevu
kwenye masuala ya Tathimini ya maji kwa mazingira kutoka Tanzania na
Australia yatawawezesha kupata maarifa na mbinu ambazo zitasaidia wao
kutekeleza vyema mipango na kusimamia masuala ya usimamizi wa mito
na vyanzo vya maji kwa maslahi mapana na binadamu, Mazingira na
miradi mingine muhimu inayotegemea maji na ikolojia nzima.

Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa Mradi huo ambaye ni Mkurugenzi wa
Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhawilishaji wa tekanolojia na Ushauri wa
kitaalamu kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili amesema utafiti huo ni moja
kati ya Miradi mitatu inayofadhiliwa na Programu ya WIOSAP nchini

Madagaska, Tanzania na Msumbiji katika kipindi cha miaka miwili na
nusu.

“Lengo la mradi huo ilikuwa ni kupunguza athari za shughuli za
kibinadamu ili kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji
wake katika Kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi Kupitia
Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji
wake kwa ufadhili wa Mkataba wa Nairobi (Nairobi Convention) fedha
ambazo ni michango ya nchi wananchama ikiwemo Tanzania” alifafanua
Prof. kashaigili.

Aidha, Prof. Kashaigili amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea
uwezo mameneja na Wataalamu kwenye nchi wananchama wa Ukanda wa
Magharibi mwa bahari ya Hindi kwenye masuala ya Tathimini ya maji kwa
mazingira na dhana ya “Kutoka kwenye chanzo hadi Baharini” (Source to
Sea) hasa katika kipindi hiki ambacho kuna changamoto kubwa za
uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji duniani.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo pia yatasaidia kujenga na kuzitazama
mbinu shirikishi ambazo zinaweza kutumika kusaidia kukabiliana na
changamoto ya athari za mtiririko wa maji kwa mazingira pamoja na
uchafuzi wa mazingira katika bahari na athari zake kwa viumbe maji.

Nae Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bwana
Wankyo Mnono amesisitiza umuhimu wa ushirikino kwa nchi zote zilizo
Magharibi mwa ukanda wa bahari ya Hindi kwakuwa ulinzi wake unahitaji
ushirikiano kwa nchi zote ili kufikia malengo ya mtiririko salama wa maji
kuelekea baharini pamoja na usalama wa bahari na viumbe maji wengine.

“Swala la ulinzi na usalama wa bahari ya Hindi linahitaji ushirikiano kwa
kila nchi katika kutelekeza makubaliano na kusimamia mtitiko wa maji
yake yanayoingia baharini, kukiwa na usimamizi kwenye nchi moja wakati
nchi nyingine ikifanya uharibifu changamoto hizi hazitaweza kumalizika
hivyo ni matumaini yangu kuwa baada ya mafunzo haya mmetengeneza
miongozo ambayo kila mmoja anakwenda kuhakikisha kwenye nchi yake
inatekelezeka” alisisitiza Wakili Wankyo.

Pamoja na mafunzo hayo pia washiriki wamepata nafasi ya kutembea
vyanzo vya maji na kuona jitihada zilizofanywa na mradi huo wa Utafiti wa
EFLOWS na Serikali kwenye eneo la Wanging’ombe Mkoani njombe na pia
kuzungumza na viongozi na Jumuiya za watumaia maji ikiwemo jumuiya ya
MBUMTILU.

Mradi wa Utafiti wa Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji Kupitia
Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji
wake katika Kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Athari
za Shughuli za Kibinadamu Tanzania (EFLOWS) unatekelezwa na Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la
hifadhi ya mazingira NEMC na wad au wengine kwa ufadhili wa
Sekretarieti ya Azimio la Nairobi.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa wakati akifunga mafunzo kwa
niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera.
Mtafiti Mkuu wa Mradi huo ambaye ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya
Uzamili, Utafiti, Uhawilishaji wa tekanolojia na Ushauri wa kitaalamu kutoka
SUA Prof. Japhet Kashaigili akieleza malengo ya mafunzo hayo.
Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bwana Wankyo
Mnono akitoa salamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.
Washiriki wa mafunzo hayo kutoka nchi nne za afrika wakiwa kwenye picha
ya pamoja na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa
mara baada ya kufunga mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo wakiangalia chanzo cha maji kwenye wilaya ya
Manging’ombe Mkoani Njombe wakiwa kwenye ziara ya mafunzo kuona
kazi zilizofanywa na mradi wa EFLOWS.
Washiriki wa mafunzo wakizungumza na Jumuiya ya watumia maji ya
MBUMTILU iliyopo Wilayani Wanging’ombe Mkoani Njombe kuona namna
jumuiya inavyoshiriki katika uhifadhi wa vyanzo vya maji.
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad